Shirika la utangazaji nchini Tanzania (TBC) limeingia mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kutangaza matangazo ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa upande wa redio.

Pande hizo mbili zimeingia mkataba huo leo Jumanne (Agosti 03) jijini Dar es saklaam katika hafla maalum iliyofanyika kwenye hoteli ya Sea Cliff na kuhudhuriwa na waandishi wa habari.

Mkataba huo wa miaka 10 una thamani ya Shilingi bilioni 3.54 na utaanza kufanya kazi kuanzia msimu ujao wa 2021-2022, ambao utaanza rasmi mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2021.

Rais wa TFF Wallace Karia amesema katika hafla hiyo kuwa, ni faraja kubwa kwa soka la Tanzania kuendelea kupata fursa ya uwekezaji mkubwa kama unaoendelea kujitokeza kwa sasa.

Amesema hatua hiyo inaendelea kuongeza chachu ya ushindani katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo kwa sasa ni miongoni mwa Ligi Kuu Bora Barani Afrika.

TBC wamesaini mkataba wa kutangaza matangazo ya soka upande wa Radio, huku Azam Media wakishinda zabuni ya kutangaza matangazo ya Ligi hiyo upande wa Televisheni kwa miaka kumi kuanzia msimu ujao wa 2021/22.

Wanane waachwa Kagera Sugar
Serikali yaanza kutafuta matokeo chanya zao la mwani