Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imechukua hatua ya kuzifungia kurasa batili za Facebook na tovuti zilizokuwa zikitumia majina ya Mke wa Rais, Janeth Magufuli na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Ally Simba alisema kuwa Mamlaka hiyo imebaini kuwepo kwa matapeli wanaotumia majina ya viongozi hao kujipatia kipato kwa njia za udanganyifu, wakilaghai kuwa viongozi hao wanatoa mikopo kupitia vikoba.

“Kwa mfano kuna matapeli walioanzisha ukurasa wa mtandao wa kijamii wa facebook kwa jina la mke wa Rais, Mama Janet Magufuli na kwa jina ma Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan wakilenga kujipatia fedha,” alisema Dk Simba.

Mamlaka hiyo pia imeifunga tovuti ya focusvikoba.wapka.mobi iliyobainika kutumia majina ya viongozi hao kutapeli.

Alisema kuwa vitendo hivyo ni uvunjifu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na kwamba mtu atakayepatikana na hatia ya makosa hayo, kwa mujibu wa kifungu cha 15 (2), atatozwa faini isiyopungua shilingi milioni 5 au kulipa mara tatu ya thamani ya kile atakachokuwa amekipata kupitia utapeli huo.

Dk. Simba alitoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kujiepusha na utapeli wa aina hiyo pamoja na kutoa taarifa kwa Mamlaka hiyo kuhusu vitendo vya utapeli kupitia mitandao.

 

 

 

Makonda kuwalipa Mamilioni watakaosalimisha silaha
Hii hapa kauli ya mwisho ya Jecha kabla ya kuanza upigaji kura Zanzibar