Watumishi wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali – OWMS, wametakiwa kutumia elimu waliyoipata na fursa ya ajira ya Serikali kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya Serikali na Taifa kwa ujumla.

Wito huo, umetolewa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende wakati akifunga mafunzo ya siku mbili Kibaha mkoani Pwani kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wapya kuhusu masuala ya kiutumishi na kuwataka kufanya kazi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma.

Amesema, ni muhimu kwa kila mtumishi kuendelea kujikumbusha masuala yote waliyofundishwa katika mafunzo hayo watakapokuwa katika vituo vyao vya kazi kwa kuwa mafunzo ndio dira kwa watumishi wote wa Serikali hasa watumishi wapya.

“Ili utumishi wenu uweze kuwa na tija, ufanisi na kuheshimika kwa Ofisi na Taifa kwa ujumla, kila mtumishi mnapaswa kufanya kazi kwa kufuata Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma kwa kuwa na tabia na mienendo inayozingatia utoaji wa huduma bora.”

“Muwe na utii kwa Serikali, utoaji wa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu Sheria za nchi na kuepuka vitendo vyote visivyofaa ikiwemo kushawishi na kupokea rushwa,” amesisitiza Dkt. Luhende.

Aidha, ameongeza kuwa OWMS inatarajia kuwa baada ya mafunzo hayo watumishi hao wataweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo hivyo kuiwezesha Serikali kunufaika na matokeo chanya yatakayopatikana na kuwa chachu katika kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake ndani na nje ya nchi.

Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo amewashukuru watumishi hao kwa umakini walioonesha katika kufuatilia mafunzo hayo ambapo amewataka kuzingatia mambo yote waliyofundishwa katika mafunzo hayo ili kufikia malengo yaliyowekwa na OWMS katika uendeshaji wa mashauri.

Amesema, mafunzo hayo yameendaliwa kwa lengo la kuwapatia nyenzo watumishi hao kwa lengo la kuwanoa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa wakati huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwa watumishi wote.

Kocha Mamelodi aitahadharisha Young Africans
Marumo Gallants kutua Dar leo