Rais wa Marekani anayeondoka madarakani , Donald Trump ametofautiana na waziri wake wa mambo ya Nje, Mike Pompeo kwa kudokeza bila kutoa ushahidi kuwa China na sio Urusi, ndiyo iliyohusika na operesheni ya udukuzi wa mtandao dhidi ya Marekani.
Katika matamshi yake ya kwanza kuhusu udukuzi huo, Trump ameandika kwenye mtandao wa Twitter akiwadhihaki wanaoiangazia Urusi na kupuuzia mbali mashambulizi hayo, ambayo shirika la Marekani la usalama wa mitandaoni lilionya kuwa yaliweka kitisho kikubwa kwa mitandao ya serikali ya kibinafsi.
Aidha, Trump amesema amefahamishwa kikamilifu kuhusu suala hilo na kuwa kila kitu kimedhibitiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje, Pompeo amesema Ijumaa usiku kuwa ni wazi kwamba Urusi ilihusika na operesheni hiyo dhidi ya Marekani.