Bodi ya Mkonge Tanzania – TSB, imejipanga kuimarisha masoko ya ndani ili kuchochea ukuaji wa uzalishaji wa Mkonge, na kuendelea kuhamasisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika Viwanda ili kuongeza thamani ya zao hilo lenye soko linaloendelea kuimarika Duniani.

Akizungumza na Waandishi wa habari hii leo Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo Saddy Kambona, amesema hatua hiyo inatokana na kuongezeka kwa matumizi ya Mkonge nchini na hivyo kuchagiza kukua kwa kilimo cha zao hilo lililingizwa kwenye orodha ya mazao ya kimkakati .

Amesema, “lakini pia ni jukumu letu kulinda viwanda vichache vilivyopo, kwa sasa takriban asilimia 70 ya mkonge unauzwa nje kama malighafi (kabla ya kuongezwa thamani), kwenye Nchi mbalimbali Duniani, na 2019 Serikali ililiingiza zao hili katika orodha ya mazao ya kimkakati na kulifanya kuwa zao la saba la kimkakati.”

“Na likaingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025 ambamo limewekwa lengo la kuongeza uzalishaji kutoka tani 36,000 zilizokuwa zinazalishwa kwa Mwaka 2020 hadi kufikia tani 80,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025, Serikali ikaiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025/2026,” amesema Kambona.

“Hii ni kutokana kugundulika kwa matumizi mapya ya Mkonge na uzalishaji wa bidhaa mpya zitokanazo na mkonge kama vile vifaa vya ujenzi(gypsum boards, Matofali,mbao, mabati, vigae), Sukari ya Mkonge, Pombe ya Mkonge, Karatasi maalum, Bio Gas, mbolea, Chakula cha mifugo , urembo, mabodi ya magari,” alifafanua Mkurugenzi huyo.

Wametishia kuipindua serikali, si kukosoa mkataba - Nape
Serikali yapanga kutekeleza miradi mikubwa ya Maji