Uholanzi imeoneshwa kuridhishwa na mazingira ya biashara na uwekezaji, demokrasia, haki za binadamu na utawala bora nchini ambapo pia wafanyabiashara wa nchi hiyo wamewekeza katika sekta za utalii pamoja na kilimo..
Hayo yamebainishwa na Balozi wa Uholanzi nchini, Wiebe de Boer wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam.
Amesema mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji nchini wafanyabiashara wengi kutoka Uholanzi wamewekeza Tanzania. “Kadhalika tumefurahishwa na kuridhishwa na demokrasia nchini, haki za binadamu na utawala bora pamoja na kufunguliwa kwa majukwaa na mikutano ya kisiasa nchini,” Alisema Balozi Boer.
Baadhi ya washiriki walioshiriki katika hafla ya maadhimisho ya Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax alieleza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendeleza uhusiano wa karibu na ushirikiano uliopo kati ya pande zote mbili kuwa Uholanzi imeendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, mifugo, uvuvi, elimu, nishati, afya, miundombinu, mawasiliano, utalii, usafiri pamoja na mafuta na gesi.
“Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji nchini, (TIC) hadi kufikia mwezi Machi, 2023 Kampuni kadhaa za Uholanzi zimewekeza Tanzania kwa kiasi cha (USD milioni 1,079.78), na kutengeneza ajira zaidi ya 15,607 katika sekta za kilimo, ujenzi, nishati, maendeleo ya rasilimali watu, mafuta na gesi, mawasiliano, utalii na usafiri,” alisema Dkt. Tax
Amesema, “Naomba kutumia fursa hii kuzialika Kampuni na wawekezaji kutoka Uholanzi kuwekeza katika fursa zilizopo na kuwekeza nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika miradi ya kimkakati na yenye maslahi mapana ya pande zote mbili.”
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, David Concar katika hafla ya maadhimisho ya Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepata mafanikio makubwa katika kuweka mazingira rafiki na mazuri ya biashara kupitia mageuzi ya kiutawala na kisheria na uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya miundombinu,” amesisitiza Dkt. Tax
Aidha, aliongeza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita zimewezesha kupungua kwa gharama za kufanya biashara nchini Tanzania na kuwezesha ufanisi na uundaji wa huduma rahisi, msingi wa kuchochea shughuli za kiuchumi, na hivyo kuongeza uwekezaji, na kuimarishwa kwa biashara nchini.