Benki ya Dunia imetenga jumla ya dola milioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mipya ya maji itakayofanyika katika Mikoa 17 na Halmashauri za miji 86 nchini.
Akizungumza mjini Singida Oktoba 24, 2019 katika warsha ya mafunzo ya uelewa juu ya utekelezaji wake Mratibu wa mradi huo Mhandisi Mashaka Sitta amesema tayari shilingi bilioni 166 bilioni zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji na kwamba malipo yatafanyika kulingana na matokeo ya kazi.
“Malipo ya utekelezaji wa mradi huu yatafanyika kulingana na matokeo ya kazi husika na tayari shilingi bilioni 166 zimekwisha kutolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu ambao unatarajia kufanyika katika mikoa 17 na halmashauri za miji 86 hapa nchini,″ amefafanua Sitta.
Amesema tayari wameanza kutoa mafunzo ya uelewa wa pamoja kwa watendaji ili kukidhi vigezo vya namna ya kupata fedha hiyo na utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi utakaokuwa na manufaa kwa nchi na jamii nzima kiujumla mara baada ya kukamilika.
Mhandisi Sitta amefafanua kuwa mafunzo hayo yameanzia katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Singida na wanatarajia kuendelea nayo katika mkoa wa Mwanza kwa lengo la kuelewa viashiria na mahitaji ya mradi vitakavyosaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji wake.
“Lengo la mafunzo haya ni kusaidia kuelewa viashiria vya mradi na kupata mahitaji husika ili kukamilisha utekelezaji wake na tayari tumefanya hivyo kwa mikoa mitatu Iringa, Morogoro na hapa Singida na mkoa unaofuata ni Mwanza ikiwa ni harakati za kuanza kwa mradi huu,” ameongeza Mhandisi Sitta.
Aidha Sitta amebainisha kuwa wanatarajia kupeleka shilingi bilion 1.36 kwa kila wilaya na kwamba Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) itafanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo kila mwaka.
Amesema sambamba na hatua za utekelezaji wa mradi huo pia wanakusudia kutatua changamoto za elimu na afya ambazo zimekuwa zikiwagusa watanzania wengi moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.