Polisi Uganda, imewakamata waandamanaji kumi na wawili waliokuwa wakipinga kupanda kwa gharama ya maisha katika eneo la Jinja, lililopo kusini-mashariki mwa nchi hiyo.
“Viongozi wanane walikamatwa na watafunguliwa mashtaka ya kuchochea ghasia siku ya Jumanne, msemaji wa polisi James Mumbi aliambia AFP.
Waandamanaji hao, wanadaiwa kuchoma matairi na kufunga barabara yenye shughuli nyingi mjini Jinja na kuwalazimu madereva wa magari kuungana nao kutaka serikali iwape ruzuku ya chakula cha msingi.
Maafisa hao wa Polisi, libidi watumie nguvu, ikiwa ni pamoja na gesi ya kutoa machozi, kuwatawanya waandamanaji.
“Bila shaka tunaunga mkono maandamano ya aina hii na Serikali lazima ichukue hatua Watu wanalala na njaa,” amesema mfanyabiashara, Solomon Wandibwa(28).
Hali ngumu inayolikabili Uganda, imechangiwa na janga la Uviko-19, na matokeo ya vita vya Ukraine, ambavyo vimeongeza bei ya nishati na chakula ulimwenguni kote.
Kulingana na takwimu rasmi za hivi punde, kiwango cha mfumuko wa bei kwa bidhaa za chakula kilifikia 13.1% kwa mwezi Mei 2022.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu 1986, amewataka raia wake kuishi kwa mpangilio badala ya kupunguza ushuru na kuongeza misaada ya serikali kwa watu walio hatarini zaidi, kama wengi wanavyotaka.
Juni 2022, mwanasiasa wa upinzani na aliyekuwa mgombea urais Kizza Besigye alifungwa jela na kushtakiwa kwa kuchochea ghasia kwa mara ya pili ndani ya mwezi mmoja, baada ya kuongoza maandamano kadhaa kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.