Kupitia ukurasa wake wa Facebook, RSA imeendelea kutoa Elimu kwa watuamiaji wa Barabara ambapo safari hii wamezungumzia juu ya jinsi mtu anavyoweza kukosa malipo ya Bima kwa kulifanyia gari lake mabadiliko ‘Modification.
RSA, inasema, inafahamu wapo baadhi ya watu hununua au kumiliki magari na baadaye kufanya mabadiliko kadhaa. Mabadiliko hayo yanaweza kuwa madogo tu kama vile badiliko la rangi (ambalo kimsingi lazima TRA wajulishwe), tairi, taa, mikanda hadi mabadiliko makubwa kama vile injini, mfumo wa taa, mafuta, bodi, nk.
Baadhi yetu huenda mbali zaidi hadi kufanya mabadiliko ya matumizi. Mathalani kama gari lilikuwa private sasa ataanza kubeba abiria au mizigo kibiashara. Wengi wetu hufanya mabadiliko haya wakati wameshakatia bima chombo husika, na bila kutambua madhara au athari zinazoweza kutokea.
Kimsingi, mabadiliko yote makubwa yanayofanywa kwenye chombo au kitu kilichokatiwa bima ni lazima kampuni ya bima ijulishwe na itoe baraka zake. Kwani baadhi ya mabadilliko haya huathiri tathmini ya hatari (assessed risk) iliyofanywa na kampuni ya bima na hivyo kupigia mahesabu ada ya bima (premium).
Kutoiarifu kampuni ya bima juu ya mabadiliko hayo wakati wa kukata bima au baada ya hapo kunapelekea mkata bima kuwa amekiuka wajibu wake wa kuingia mkataba kwa nia njema (duty of utmost good faith) kati yake na kampuni ya bima, kwa kuweka wazi kila taarifa na hali inayohusiana na chombo kinachokatiwa bima.
Sasa iwapo itatokea chombo kilichokatiwa bima kimefanyiwa mabadiliko (modification) na kampuni ya bima haikuarifiwa na chombo hiki kikaja kupata ajali, kampuni ya bima ikafahamu kuhusu mabadiliko hayo, basi kampuni ya bima itakuwa na haki ya kukataa kumlipa mhusika kwa kigezo cha kukiuka wajibu wa nia njema.
Kwa maana nyingine, mwenye chombo anakuwa aliuficha ukweli kampuni ya bima na hivyo kufanya mkataba kati yake na kampuni ya bima kuwa batili ambapo kanuni hii imepata kusemwa au kutumika katika kesi kadhaa duniani, maarufu sana ikiwa ile ya Carter v Boehm; Pan Atlantic Insurance Company Ltd Vs Pine Top Ins. Co. (1995) A.C 501, na Hajji Kavuma v First Insurance Company Ltd (Civil Suit-2013/442) (2018), UGCommC 65 (07 May 2018) ikiwa ni baadhi tu ya kesi.
Hivyo, tujitahidi kutoa taarifa kwa kampuni ya bima kila tunapofanya modification kwenye magari yetu.
Ni imani yetu makala hii imekuongezea maarifa
RSA Admin – Usalama Barabarani ni Jukumu Letu Sote.