Inadaiwa kuwa watu milioni 1.4 wanaishi na virusi vya ukimwi nchini Tanzania huku idadi ndogo ya wananchi ikijitokeza kwenda kupima afya zao.
Taarifa kutoka taasisi ya Egpaf – Boresha Afya imesema kuwa hadi kufikia Oktoba 2016 asilimia 70 ya watu wanaoishi na VVU ndio waliopima kufahamu hali zao na maendeleo ya afya.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Egpaf, Jeroen Van’t Pad Bosch ambapo amesema kuwa zinahitajika juhudi kubwa ili Tanzania ifikie lengo la asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU kupima afya na kujitambua.
Amesema kuwa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) limetoa Dola129 milioni (zaidi ya Sh260 bilioni) kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Egpaf – Boresha Afya unaotekelezwa katika mikoa sita hapa nchini kwa ajili ya mradi wa upimaji VVU.
Aidha, amesema kuwa Egpaf inafanya kazi kwa ushirikiano na vituo vya afya vya Serikali na mashirika binafsi katika mikoa hiyo kwa lengo la kuhakikisha watu 170,000 wanapimwa VVU.
“Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake wanaopima VVU ni wengi kuliko wanaume, ambapo asilimia 82 ya wanawake wanaoishi na VVU nchini tayari wamepima na wanafahamu afya zao huku kwa wanaume wakiwa wachache,” amesema Jeroen
Hata hivyo, Meneja Mradi wa Usaid – Boresha Afya kutoka Ofisi ya Egpaf mkoani Arusha, Dkt. Leo Haule amesema kuwa wamekuwa wakitengeneza huduma rafiki kwa vijana ili wapate huduma ambayo itawaridhisha na kufanya wasiache kutumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi.