Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni (WHO), liko kwenye mchakato wa kubadilisha jina la ugonjwa wa ndui ya nyani au Monkeypox ili kuepusha unyanyapaa kwa watu walidhurika na ugonjwa huo.
Msemaji wa WHO, Fadéla Chaib ameyasema hayo jijini Geneva nchini Uswisi wakati alipoulizwa swali na waandishi wa Habari kuhusu mchakato huo ambapo amesema mtu yeyote wa kawaida, taasisi za elimu, mashirika ya kiraia anakabirishwa kupendekeza jina jipya, kupitia jukwaa la wavuti ya WHO.
Bi. Chaib amesema, “Ni wajibu wa WHO na mfumo wake wa kubainisha magonjwa kufanya hivyo, na kwamba katika kupatia majina magonjwa, tutafanya mashauriano ya wazi kupata jina jipya la ugonjwa wa ndui ya nyani.”
Hata hivyo ameongeza kuwa, hadi sasa hakuna muda kamili wa kupata jina hilo na kwamba iwapo jina jipya likipatikana umma utajulishwa na kwa mujibu wa WHO, ndui ya nyani iliwekwa kwenye kundi la magonjwa ya kitropiki yanayopuuzwa, yaani NTDs..
Kuhusu swali, ni kwa nini jina la ndui ya nyani linaonekana kuwa linanyanyapaa na kutaka libadilishwe, Bi. Chaib amesema kwa miaka kadhaa imekuwa ni utamaduni wa WHO kuhakikisha majina ya magonjwa hayaleti unyanyapaa kwa ukanda, nchi, kabila au mnyama na kwamba kwa sasa ni zamu ya ndui ya nyani.
Ugonjwa wa ndui ya nyani, uligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1958, na umejikita zaidi katika nchi za Afrika hadi mlipuko wa mwaka huu wa ndui ya nyani ambapo wagonjwa wengi wameripotiwa kutoka nchi za Ulaya.