Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), limetoa msaada wa mahitaji kwa Mahabusu na Wafungwa katika Gereza la Mpanda Wilayani Mpanda na Kalilankulukulu la Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi, wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 29.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Ofisa Hifadhi Mwandamizi wa UNHCR Mkoa wa Kigoma Peter Muriuki, amesema shirika hilo linatambua kuwa magereza ni mdau muhimu katika suala la utoaji haki na kurekebisha tabia.
Amesema, “Tumetoa vifaa vyenye thamani ya shilingi 29,100,000 katika magereza mawili, ambapo gereza la mahabusu ya Mpanda vifaa vyenye thamani ya shilingi 22,425,000 na gereza la kilimo Kalilankulukulu shilingi 6,675,000, vifaa vya wafungwa na vifaa vya Tehama ili kusaidia shughuli za kiofisi.”
Naye, Afisa Hifadhi mshiriki UNHCR Kigoma, Rehema Msami amesema msaada walioutoa katika magereza hayo kuwa ni Kompyuta ya kisasa na Printa, kifaa kinachodhibiti matumizi ya umeme, na magodoro, Kanga, Dawa za kuzuia mbu, Dawa za meno, viatu, ndoo na taulo za kike.
Akizungumza wa niaba ya mkuu wa magereza Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Akley Mkude amelishukuru shirika hilo kwa kuona kuwa wafungwa wanahitaji msaada wa kibindamu.