Wakala wa Nishati Vijijini – REA, umesema Juni 2024 wanatarajia kuhitimisha safari ya kupeleka umeme vijiji vyote nchini na kwamba utakuwa umekamilisha kabla ya lengo kutokana na kupata usaidizi mkubwa wa Serikalini pamoja na Wadau wa maendeleo.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo, Mhandisi Jones Olotu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Hassan Saidy ambaye ameeleza kuwa, Tanzania Bara kuna vijiji 12,318 ambapo hadi kufikia leo vijiji 11,313 vimeunganishwa na umeme huku vijiji 1,005 vilivyobakia wakandarasi wapo kazini kukamilisha kazi ya kuunganisha na kuwasha umeme.

Mhandisi Olotu amesema, kati ya vitongoji vilivyopo nchini 64,760 tayari vitongoji 28,659 vimefikiwa na umeme, vitongoji 36,101 bado wapo mbioni kuvifikishia umeme kwa kuwa mipango tayari imeshaandaliwa. Mhandisi Olotu amebainisha kuwa,mwaka 2030 malengo yao ni kuhakikisha kuwa, vitongoji vyote vimepata umeme nchini.

Amesema, miongoni mwa changamoto ambazo wanakabiliana nazo ni uharibifu wa miundombinu ikiwemo uharibifu wa nguzo kutokana na shughuli mbalimbali za wananchi katika maeno ambayo wanachoma moto hovyo na kwamba wataendelea kutoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa wanakuwa mstari wa mbele kuilinda miundombinu ya nishati ili iweze kuwanufaisha.

Ameongeza kuwa, amesema, Wakala wa Nishati Vijijini – REA, ulianzishwa kwa Sheria ya Nishati Vijijini Na.8 ya mwaka 2005 na kuanza kazi rasmi mwezi Oktoba 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa iliyokuwa Sera ya Nishati ya mwaka 2003. Sheria ya Nishati Vijijini pamoja na kuanzisha wakala, pia imeanzisha Bodi ya Mfuko wa Nishati Vijijini.

Awali, akizungumzia kuhusiana na vikao kazi hivyo ambavyo vinazikutanisha taasisi na mashirika mbalimnali ambayo yapo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Afisa Habari na Mawasiliano wa ofisi hiyo, Sabato Kosuri amesema,lengo ni kuzikutanisha taasisi za umma mbele ya umma kupitia wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Kosuri amesema,vikao hivyo vinazipa nafasi taasisi hizo kuelezea kwa kina walipotoka, walipo, wanapoelekea na mafanikio yao ili umma ambao ni wamiliki wakuu waweze kutambua yanayojiri.

Wananchi wamshangaza Naibu Waziri
TAWA kushughulikia tatizo uvamizi wa Tembo uraiani