Aprili 15, 2023 Kikosi Maalum cha Wanamgambo nchini Sudan cha RSF, kilitangaza kuchukua udhibiti kamili wa Ikulu ya rais, makazi ya mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum nchini Sudan.
Katika taarifa yake RSF ilisema imechukua pia udhibiti wa viwanja vingine viwili vya ndege, kwenye mji wa kaskazini wa Merowe na mji wa El-Obeid ulioko upande wa kusini mwa nchi hiyo.
Kikosi hicho cha RSF kinachoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu kama Hemedti, kilisema jeshi lilizingira moja ya kambi zake na kufyatua risasi kwa kutumia silaha za kivita huku
vyama vya kiraia vya Sudan vikitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano yaliyozuka baina ya vikosi hivyo viwili.
Baadhi ya wananchi wa Sudan wakiondoka kupisha mapigano yanayoendelea jijini Khartoum. Picha ya Sudan Tribune.
Vyama hivyo vilisaini makubaliano ya awali ya kugawana madaraka na jeshi la nchi hiyo pamoja na kikosi cha RSF lakini kutokana na hali hii vikarudi nyuma na kutoa wito kwa wadau wa kimataifa na kikanda kuchukua hatua haraka kuzuia umwagaji damu.
Badaye, mara baada ya taarifa hizo mapigano makali yakazuka katika mji mkuu wa Sudan licha ya kusimama kwa saa nyingi ili kupisha shughuli za mahitaji ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kuwahamisha majeruhi, katika siku ya pili ya vita hivyo vilivyosababisha wafanyakazi watatu wa Umoja wa Mataifa kuuawa.
Mapigano haya kati ya vikosi vyenye nguvu na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yakazua malalamiko ya kimataifa na wasiwasi wa kikanda, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa mpaka na majirani wa nchi za Misri na Chad.
Hali ilivyo katika jiji la Khartoum. Picha ya Africanews.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za vyombo vya Habari vya kimataifa, milipuko mizito na milio ya risasi ilisikika katika vitongoji vya kaskazini na kusini mwa mji mkuu Khartoum wenye wakazi wengi huku vifaru vikiunguruma mitaani na ndege za kivita zikiunguruma angani.
Mapigano hayo yakaendelea baada ya usiku wa kuamkia Jumapili (Aprili 16, 2023), wakati Wasudan wakijifungia majumbani mwao kwa hofu ya mzozo wa muda mrefu ambao unaweza kuiingiza nchi katika machafuko makubwa zaidi, na kuondoa matumaini ya muda mrefu ya mpito kwa demokrasia inayoongozwa na raia.
Hata hivyo baada ya wafanyakazi watatu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP kuuawa shirika hilo lilitangaza kusitisha shughuli katika nchi hiyo na hali hii pia ikafanya kuongezeka kwa ghasia na kuharibu mpango wa wiki kadhaa za vita vya kuwania madaraka kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake, Mohamed Hamdan Daglo ambaye anaongoza RSF yenye silaha nzito huku Kila mmoja akimshutumu mwenzake kwa kuanzisha vita.
Jenerali Mohamed Hamdane Daglo, “Hemedti” wa Kikosi cha Msaada wa Haraka – FSR (kulia), na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane anayeshikilia mamlaka tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021 (kushoto). Picha ya The wire.
Siku hiyo nayo ikapita na Aprili 18, 2023 ikatoka ripoti kuwa mapigano kati ya jeshi na wanamgambo nchini Sudan yamesababisha vifo vya takriban watu 200 na wengine 1,800 kujeruhiwa, mali kuharibiwa na majengo ya Hospitali kubomolewa na makombora hali iliyopelekea kukwamisha misaada na usaidizi kwa waathiriwa.
Sauti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ikasikika yeye akazitaka pande zinazopigana nchini humo kusitisha uhasama mara moja na kusema ongezeko la mzozo kati ya jeshi na makundi ya kijeshi, wakiongozwa na majenerali wapinzani, unaweza kuleta athari kubwa nchini humo na maeneo jirani na ukanda huo.
Vurugu hizo, ambazo zilizuka siku ya Jumamosi Aprili 15, 2023 zimekuwa zikiendelea kwa muda wa siku ya nne hadi leo huku idadi ya vifo vya watu vikiongezeka hadi kufikia vifo vya watu wasiopungua 200 hali iliyoleta simanzi na majonzi kwa Taifa hilo lenye mizozo ya mara kwa mara.
Taarifa ya kushtua ni kwamba, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anasema hadi sasa mapigano hayo ya nchini Sudan. Picha ya Africanews.
Mapigano hayo, yanazuka kufuatia vita vya kugombania madaraka kati ya majenerali wawili walionyakua mamlaka katika mapinduzi ya mwaka 2021, ni Mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, na Makamu wake, Mohamed Hamdan Daglo yeye ni kamanda anayeongoza kikosi cha RSF chenye nguvu na anayesema amesitisha mapigano kwa saa 24.
Lakini leo ni siku nyingine ambapo Miripuko ya risasi na mabomu, imeendelea kusikika katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum licha ya tangazo la RSF la kudai kusitisha mapigano hatua ambayo imepelekea wito wa kimataifa wa kukomesha uhasama uliosababisha kuongezeka kwa uasi, vifo na uharibifu.
Lakini Kamanda wa RSF, Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, anatangaza kuunga mkono jitihada ya kimataifa ya kusitisha mapigano huku upande wa jeshi la Sudani ukionekana kutotilia maanani mpango huo.
Wasudan wakingojea usafiri kuelekea nje ya jiji la Khartoum lenye mapigano. Picha ya Liberation.
Taarifa ya kushtua ni kwamba, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anasema hadi sasa mapigano hayo ya nchini Sudan, yaliyopamba moto katika mji mkuu wa Khartoum na maeneo mengine, hayana dalili ya kusitishwa.
Nani ataingilia ugomvi huu na kuumaliza? Afrika karibu maeneo mengi yana migogoro, ufisadi, uchu wa madaraka, vilio vingi ni juu ya umasikini licha ya uwepo wa rasilimali nyingi tulizobarikiwa na MUNGU, vita, machafuko, ongezeko la gharama za maisha na mauaji ya kutisha, hivi ni nani aliyeturoga?
WAKATI NI SASA WAAFRIKA TUAMKE.