Siku 100 za uongozi wa Rais John Magufuli zimetoa picha tofauti inayompandisha zaidi na kuongeza kiwango cha kukubalika kwa wananchi huku kiwango cha aliyekuwa mpinzani wake mkubwa, Edward Lowassa ukiporomoka, tafiti zimebaini.

Rais Magufuli 2

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na kampuni ya Mwananchi Communication Limited, iliolenga katika kubaini asilimia za wananchi ambao wangempigia kura Rais Magufuli au Lowassa endapo uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, ungefanyika wakati huu.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliotumia sampuli ya watu 1200, Dk. John Magufuli alipata asilimia 74.5, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya asilimia 58.5 alizopata kupitia uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.

Wakati kiwango hicho kikipanda, utafiti huo umeonesha kuwa hali sio nzuri kwa Lowassa aliyegombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo akiungwa mkono na vyama vya upinzani Ukawa. Kukubalika kwa Lowassa kumepungua kwa takribani asilimia 20.

Lowassa amepata asilimia 20.1, kiasi ambacho ni pungufu kwa kulinganisha na asilimia 40 alizopata katika uchaguzi uliopita.

Kwa mujibu wa utafiti huo, vijana ambao walikuwa wakimsapoti Lowassa kwa asilimia kubwa zaidi, hivi sasa wengi wao wamehamia kwa Magufuli. Imebainika kuwa endapo uchaguzi huo ungefanyika wakati huu, asilimia 73 ya vijana wenye umri kati ya miaka 26 na 35 waliofikiwa na utafiti huo, wangempigia kura Magufuli.  Kadhalika, asilimia 72.8 ya watu wenye umri kati ya miaka 36 na 45 wameonesha kuwa wangemuunga mkono Dk. Magufuli.

 

TASWA Yalaani Kitendo Cha Mwinyi Kazimoto
Dimitri Payet Awafunga Midomo Viongozi Wa Man City