Rapa Zaiid ambaye ni mmoja wa wanafamilia wa ‘Sisi Sio Kundi’, amesimulia namna ambavyo wimbo wake ‘Wowowo’ ulivyomletea shida kwa wasanii wenzake.

Akifunguka kwenye mahojiano maalum na Dar24, rapa huyo ambaye hivi karibuni alibadili mtindo wa uimbaji wake, alisema kuwa kutofungiwa kwa wimbo wake na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), kuliwapa shida baadhi ya wasanii wenzake ambao nyimbo zao zilifungiwa.

Alieleza kukumbuka namna ambavyo Gigy Money ambaye wimbo wake ‘Papa’ ulifungiwa, alivyotaka kujua sababu za kuufanya ‘Wowowo’ kutofungiwa.

“Kibaya zaidi hata ndugu zangu waandishi walikuwa wanautaja sana kwenye vikao vya BASATA, ‘mbona mmefungia hizi, mbona hii bado?,” alisema.

“Nakumbuka hadi Gigy Money akahoji kabisa mbona mmenifungia mimi lakini ‘Wowowo’ haijafungiwa” aliiambia Dar24.

Hata hivyo, rapa huyo alidai kuwa hakuchukuliwa vibaya hali hiyo ya wasanii wenzake kuutaja wimbo wake kama mfano wa zilizosahaulika kwenye kufungiwa, bali alichukulia kama kutofautiana kimtazamo juu ya wimbo huo.

Hivi sasa, Zaiid anafanya vizuri na wimbo ‘Picha’ ambao umefuata mkondo wa ‘Wowowo’ na kuacha njia ya hip hop aliyokuwa amezoeleka kuifanya.

Zaiidi amedai kuwa uamuzi wa kufuata njia hiyo unatokana na mapokeo makubwa ya ‘Wowowo’ iliyompa michongo mingi zaidi ya wimbo wake wowote.

Video: Hakuna kifo kibaya kama kifo cha moto na maji, hizi ni 'beach' hatarishi duniani
Usher ashusha albam mpya ‘A’, isikilize hapa