Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia mipaka na majukumu yao katika utendaji wa kazi ili
kuepusha migogoro na miingiliano katika kuwahudumia wananchi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Amesema, ni lazima watendaji na viongozi wote wa kisiasa kufanya kazi kwa pamoja na kufanya mazungumzo ya kujenga kwa manufaa ya wananchi panapotokea hoja au mitazamo tofauti katika
utekelezaji.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi viongozi hao kutambua lengo kuu katika nyadhifa zao ni kuwaletea wananchi maendeleo na siyo migogoro baina yao hivyo ni muhimu kuheshimiana, kuwajibika, kushirikiana kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuondoa vikwazo vyovyote
vinavyoweza kukwamisha miradi hiyo.
Pia amehimiza ushirikiano baina ya Madiwani na Wakurugenzi wa Halmashauri na kuondokana na tabia ya Madiwani kutoa maazimio dhidi ya Wakurugenzi pamoja Wakurugenzi kutowaheshimu Madiwani.