Maelfu ya Watu wameandamana nchini Israeli, kupinga kufutwa kazi kwa Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant mara baada ya kuitaka Serikali kuachana na mpango tata wa kuifanyia mageuzi idara ya Mahakama.
Hayo yamejiri baada ya Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu kumsimamisha kazi Waziri wa Ulinzi nchini humo ambapo waandamanaji walifunga barabara kuu jijini Tel Aviv, huku wengine wakiwasha moto kuonesha hasira yao, baada ya uamuzi wa Netanyahu.
Inaelezwa kuwa, waandamanaji zaidi ya Laki mbili, walijitokeza kupinga mageuzi hayo na kufutwa kazi kwa Waziri huyo, wakisema mchakato huo wa Mahakama ni lazima ukomeshwe kwa sababu unaigawa nchi.
Miongoni mwa mabadiliko hayo, ni kutoa kipaumbele kwa wanasiasa na serikali, kuunda Kamati itakayowateuwa Majaji wa Mahakama.
Hatua hiyo pia imesababisha kujiuzulu kwa Asaf Zamir, mwanadiplomasia wa Israeli jijini New York, ambaye amesema hawezi kuendelea kuiwakilisha serikai hiyo.