Wachezaji kumi wa timu ya taifa ya Eritrea waliokuwa wameenda kucheza mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Botswana wamekataa kurejea nyumbani. Maafisa nchini humo wanasema wachezaji hao sasa wanataka kupewa hifadhi huko.

Wachezaji hao walizuiliwa na polisi baada yao kukataa kuabiri ndege iliyofaa kuwarejesha nyumbani. Wanadaiwa kukataa kurudi nyumbani hata baada ya kujaribu kushawishiwa na balozi wa Eritrea nchini Botswana.

Eritrea ilishindwa 3-1 kwenye mechi hiyo nchini Botswana na ikabanduliwa kutoka kwenye kinyang’anyiro hicho cha kufuzu kwa Kombe la Dunia kwani ilikuwa imelazwa 2-0 mjini Asmara mechi ya mkondo wa kwanza.

Wachezaji wa Eritrea wamekuwa wakitoweka mara kwa mara na kukataa kurejea nyumbani. Kisa kinachokumbukwa sana ni kile cha mwaka 2013, pale Uganda ilipowapa hifadhi wachezaji 13 wa Eritrea na daktari wa timu baada yao kukataa kurejea nyumbani baada ya kucheza mechi.

Afisa mkuu wa Shirikisho la Soka la Botswana amesema bado haijabainika ni kwa nini wachezaji hao walikataa kuondoka na wenzao.

Hata hivyo, ripoti katika gazeti la Botswana la The Voice inasema wachezaji hao wanaogopa kulazimishwa kujiunga na jeshi wakirejea nyumbani. Aidha, inadaiwa sasa wanaogopa huenda wakashtakiwa kwa uhaini iwapo watakubali kurudi nyumbani.

Gazeti hilo lilimnukuu makamu wa rais wa Shirikisho la Soka la Botswana Basadi Akoonyatse akisema iligunduliwa wachezaji hao hawakuwa kwenye vyumba vyao hotelini Jumatano asubuhi.

“Polisi walifahamishwa na baada ya msako wakatapikana wakizurura katika mji wa Francistown, wakidai walikuwa wakitafuta kituo cha Shirika la Msalaba Mwekundu kuomba usaidizi … wa kupata hifadhi Botswana,” alisema. Mwakilishi wa wachezaji Dick Bayford aliambia shirika la habari la Reuters kwamba alipokea habari kuhusu juhudi za kuwaondoa wachezaji hao kutoka Botswana kwa nguvu.

Eritrea imekuwa ikituhumiwa kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu. Ripoti ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilisema taifa hilo huwa na visa vya watu kuteswa na kufanywa watumwa.

Nchi hiyo imetuhumiwa na UN kwa kulazimisha raia kujiunga na jeshi na kuua watu wanaojaribu kutorokea ng’ambo. Serikali ya Eritrea imepuuzilia mbali madai hayo ya UN ikisema hayana msingi.

 

Simba Yawatakia Watanzania Uchaguzi Mwema
Lowassa Ashangaa Alichokisema Rais Kikwete