Wachimbaji wadogo watano katika mgodi wa Nyangarata wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wameokolewa baada ya kuishi ndani ya shimo kwa siku 41 wakiwa wamefukiwa na maporomoko ya mgodi huo.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, watu hao walikuwa miongoni mwa watu sita walionasa katika ajali ya maporomoko yaliyotokea Oktoba 5 mwaka huu.

Kamanda Kamugisha alieleza kuwa watu waliokwenda kuiba mchanga wa dhahabu ndani ya mgodi huo ndio waliobaini kuwepo kwa watu hao ndani ya mgodi baada ya kusikia kilio cha kuomba msaada.

Kwa mujibu wa waathirika hao, walikuwa watu sita walionasa lakini mmoja kati yao alifariki baada ya kukataa kula wadudu na magome ya miti.

Walieleza kuwa wao walifanikiwa kuishi katika kipindi hicho kwa kula magome ya miti na kwamba walikuwa wanatumia kofia zao kuchota maji yaliyokuwa yanatiririka na kuyanywa.

Kamanda Kamugisha aliwataja watu hao kuwa ni Chacha Wambura, Amosi Muhangwa, Joseph Burulwa, Msafiri Gerald na Wonyiwa Moris.

“Tulikuwa tukitumia miti inayojengea kingo za mashimo kama chakula pamoja na wadudu wadogo wadogo ndani ya mashimo hayo, hasa mende. Pia tulikuwa tukitumia kofia zetu ngumu kukinga maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu ya ardhi ingawa yalikuwa machafu,” alisema Chacha Wambura ambaye ni mmoja wa wahanga hao huku akimtaja mwenzao aliyepoteza maisha kwa jina la Musa.

Waathirika hao wamefikishwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama na wanaendelea kupata matibabu.

Mganga mfawithi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Joseph Ngowi alieleza kuwa wanaendelea kuwapa matibabu yakiwemo ya kisaikolojia na lishe ili kuhakikisha wanarejea katika hali yao ya kawaida.

Ali Kiba Aeleza Kwanini Hakupost Kumpongeza Diamond, Vanessa
Donald Trump ‘Achafua Hewa' Tena Na Hili Kuhusu Misikiti ya Marekani!