Wadau wa sekta ya afya wamesema utungwaji wa sheria ya uvunaji, usimamizi na utunzaji wa viungo vya ndani vya binadamu utasaidia kuanzishwa kwa benki za viungo nchini, hivyo kuboresha matibabu ya kibingwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani -WHO na Shirika la Hispania la Upandikizaji wa Viungo (ONT), mwaka 2021 figo ni kiungo kinachoongoza kwa kupandikizwa watu kikifuatiwa ini na moyo.

Takwimu hizo, zinaonyesha kwa mwaka huo inakadiriwa viungo 144,302 vilipandikizwa ulimwenguni ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.3 la mwaka 2020.

Mchanganuo huo, unaonyesha viungo vilivyopandikizwa mwaka huo figo ni 92,532, ini (34,694), moyo (8,409), mapafu (6,470), nyongo (2,025) na utumbo mwembamba (172).

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema wapo katika mchakato wa kuandaa muswada wa kuruhusu watu kuchangia viungo vya ndani ikiwamo figo.

“Lakini sisi hatuna sheria nchini ya kuchangia viungo vya ndani, ndio tunataka kuitunga kwa hiyo tunahitaji kutoa elimu…unaweza ukatoa figo yako moja na ukaishi vizuri tu,” alisema Waziri Ummy wakati anazindua jengo la Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

8

Akizungumza na Mwananchi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Dk Faustine Ndugulile alisema ni wakati muafaka wa kutungwa kwa sheria hiyo kwa sababu huduma hizo za upandikizaji wa viungo ikiwamo figo, ute wa mifupa na kubadilisha vipandikizi mbalimbali katika mwili zimeboreshwa.

“Teknolojia imekuwa lazima iambatane na sheria zake. Na dunia imekuwa sasa hivi kuna wanawake ambao hawapati ujauzito, katika dunia kuna mbegu hata za kiume na hata mayai ya kina mama,” alisema Ndugulile.

“Hatujaweza kuwa na benki ya mayai ya wanawake wala mbegu za wanaume kwa sababu hakuna sheria inayoruhusu kufanya hivyo. Huko duniani kuna benki ya viungo mtu amepata ajali anaandika kabisa mimi nikifariki dunia viungo vyangu vivunwe viweze kutumika kwa watu wengine,” alisema Ndugulile.

Alisema pia nchi nyingine duniani kuna benki ya maziwa ya wanawake ambao inaweza kuwasaidia wanawake waliojifungua lakini hawana maziwa ya kutosheleza.

Dk Ndugulile alisema kuna vitu vingi ambavyo vipo vinavyohitaji sheria itakayosimamia uvunaji, utunzaji na matumizi ya viungo na tissue za binadamu.

Alisema kutokuwepo kwa sheria kunaweza kusababisha watu kufanya biashara haramu ya viungo vya binadamu kama ilivyotokea nchini India.

Alipoulizwa kama utungwaji wa sheria hiyo hautahamasisha watu kuuza viungo vyao, Dk Ndugulile alisema sheria itaweka utaratibu ninani atoe viungo na nani hawezi kutoa viungo.

Alisema misingi ya WHO inakataza ufanyaji wa biashara ya viungo sawa na uchangiaji wa damu ambao mtu anayechangia huchangia kwa ajili ya kumsaidia muhitaji na si kufanya biashara.

“Tukiwa na utaratibu mtu amepata ajali anaona kuwa hatoweza kuishi na akatoa ruksa viungo vyake vinaweza kuvunwa,” alisema Dk Ndugulile ambaye pia ni mbunge wa Kigamboni (CCM).

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndilana alisema utungwaji wa sheria hiyo utawezesha kuendana na mpango wa Serikali wa utoaji wa huduma za kibobezi nchini.

“Hii itasaidia sana waliopata matatizo ya viungo wanahitaji upindikizaji kupata viungo hivyo kwa sababu sheria itakuwa imeeleza jinsi ya kusimamia uchangiaji wa viungo hivyo,” alisema Dk Ndilana.

Alisema kwa nchi zilizoendelea ni jambo la kawaida kwa baadhi ya watu kuandika wosia wake kwamba iwapo akifariki dunia viungo vyake vitumike kuwasaidia watu wengine wenye shida za viungo.

Chanzo @ Mwananchi.

CHADEMA waitaka CCM kukamilisha miradi iliyokwama
Botswana, Namibia waondosha starti la paspoti