Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Mkuranga, Mkaguzi wa Polisi, Claudia Mselle amewaasa Wahitimu wa Darasa la saba kutambua wajibu wao katika jamii na kudumisha nidhamu zaidi, kwani wanaenda kukutana na jamii ambayo ipo uraiani, hivyo wasijihusishe na ushiriki wa vitendo vyovyote vya kiuhalifu.
Mselle ameyasema hayo wakati akizungumza na kuwapa elimu Wanafunzi wa Shule ye Msingi Mwandege na Kipara zilizopo Kata ya Mwandege Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani na kudai kuwa uhuru wanaoanza kuupata leo hauwafanyi kujiona wamemaliza maisha ya kimasomo kwakuwa bado wanahitaji kusonga mbele.
Amesema, wao bado ni watoto kwa mujibu wa sheria na kuwakumbusha Kifungu cha Sheria namba 15(1)(2)(3) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 na marejeo yake ya mwaka 2022 kwamba mtoto mwenye miaka 12 iwapo akifanya uhalifu wowote anatambulika kama muhalifu na anashitakiwa kwenye Mahakama za watoto.
Aidha, Inspekta Mselle pia aliwataka wahitimu wa kike kuwa waangalifu na kutodanganyika kwani mimba za utotoni zina madhara makubwa kiafya na kiakili, huku Wahitimu wa kiume wakielezwa kuwa wao ni wanaume kamili na wasikubali mtu yoyote kuwabadilisha akili zao na kuwafanyia ukatili.