Katika hali isiyokua ya kawaida kwa wananchi kusogelea mali ya rais, nchini kenya watu wanne wamekamatwa kwa njama ya kujaribu kumuibia Rais Uhuru Kenyatta kipande chake cha ardhi.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, wanne hao walikamatwa wakishukiwa kupanga njama ya kutaka kuuza shamba hilo lililo katika mtaa wa kifahari wa Karen.

Wanne hao ambao ni Mohamed Muhammud, James Opere, Jonah Tuuko na Samakin Lesingiran walifikishwa mahakamani jijini Nairobi kwa kesi hiyo na wataendelea kusalia kuzuizini ili kuruhusu polisi kuendelea na uchunguzi.

Hakimu anaesikiliza kesi hiyo, Jane Kamau alisema watu hao wanaweza kuachiliwa leo kwa dhamana ya KSh 30, 000 sawa na zaidi ya shilingi laki 4 ya kitanzania kila mmoja.

Upande wa mashtaka ulisema kipande hicho cha ardhi kiko katika eneo la Windy Ridge na wanne hao waliingia katika shamba hilo kwa lazima Januari 3 na kutafuta mipaka ya shamba hilo huku afisa anayeendesha uchunguzi akiiambia mahakama kuwa nia yao ni kuliuza.

Alisema licha ya kuwa shamba hilo linamilikiwa na Rais Kenyatta, kuna hati miliki feki ambayo watu hao wanaitumia kuwahadaa wanunuzi ambalo ni kosa jingine kisheria

Aliitaka mahakama kumpa muda wa kuendeleza uchunguzi huku wanne hao wakizuiliwa ili afaulu kupata aliye na hati miliki hiyo feki.

Taarifa za kisa hicho zimeibua hisia tofauti mtandaoni wengi wakihoji ni vipi walipata nguvu za kujaribu kumuibia rais na hapa ndipo ule msoemo ‘ukistaajabu ya Musa, utayaona ya Firauni’.

Dkt. Biteko: Msiwatenge wachimbaji wanawake
Mapya yaibuka kujiuzulu kwa Ndugai "Ni siasa..."