Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa wiki ya maonesho ya nne ya viwanda ya nchi za SADC ni fursa pekee ya kutangaza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Ameyasema hayo leo mchana (Jumanne, Agosti 6, 2019) wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mabanda kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo ambayo yalifunguliwa jana na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, yanafanyika katika maeneo matatu ambayo ni ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, viwanja wa Gymkhana na viwanja vya Karimjee.
“Nimekuja kufanya ufuatiliaji wa maandalizi ya mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC, nimekuta yanaendelea vizuri. Nimekuja kuangalia mwitikio wa wajasiriamali wa pande zote mbili za Muungano pamoja na wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa SADC, na pia mwitikio wa wananchi wetu ukoje,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema fursa hiyo ni muhimu kwa Watanzania kuonesha bidhaa za ndani ili wageni wanaokuja wajue kuna bidhaa zipi zinazozalishwa nchini.
Amesema kuwa mbali ya fursa ya masoko, Tanzania inayo pia fursa ya kupata teknolojia mpya na za Kisasa ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa viwanda vya usindikaji bidhaa mbalimbali. “Tumeona utaalamu unaotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali, hii maana yake ni kwamba tunajifunza na teknolojia zinazotumika,” amesema.
“Tunayo fursa ya kukaribisha viwanda kutoka nje ya nchi, wote hapa wameleta bidhaa zao. Pia tunawakaribisha waje waanzishe viwanda kwa ubia na Watanzania. Sisi tunayo ardhi, tunazalisha mazao mengi tu, kwa hiyo mbia wa nje anaweza kuunganisha mtaji na Mtanzania na wakajenga kiwanda hapa nchini,” ameongeza Majaliwa.
Mbali ya fursa za kiuchumi kwao binafsi, Waziri Mkuu amewataka washiriki wa maonesho hayo, watangaze vivutio vya utalii vilivyopo nchini ambavyo vitasaidia kuwafanya wageni wanaoshiriki mkutano huo watamani kubaki nchini na kuvitembelea.
“Watanzania tutumie nafasi hii kutangaza vivutio vingine tulivyonavyo. Mbuga za wanyama tunazo nyingi, tunao Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika na huwezi kuupanda kutokea popote. Ili uupande, ni lazima uje Tanzania,” amesema.
“Pia tuna eneo maarufu la Olduvai Gorge ambalo ni chimbuko la binadamu wa kwanza duniani, na hili liko eneo liko Ngorongoro. Tuna fukwe nzuri, zenye mchanga mzuri ambazo ukikaa wala huwezi kuchafuka, zina urefu wa zaidi ya km. 1,400 kutokea Tanga hadi Mtwara,” ameongeza.
Awali Waziri Mkuu alifanya kikao na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Utumishi na Utawala Bora, Viwanda na Biashara wa SMT, Viwanda, Biashara, Wazee na wa Zanzibar (SMZ), Naibu Mawaziri wa TAMISEMI, Mambo ya Nje na Mifugo na Uvuvina kuwapa maelekezo ya kuboresha maandalizi hayo. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Makatibu Wakuu wa wizara hizo.