Jeshi la Polisi Mkoani Geita, linawashikilia watu tisa wakiwemo viongozi wa kisiasa kwa tuhuma za kulima bangi katika eneo la msitu wa hifadhi ya Mienze, iliyopo kijiji cha Wavu kata ya Shabaka Wilayani Nyang’hwale.
Watu hao, wamekamatwa kufuatia operesheni inayofanywa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame kwa kushirikiana na jeshi la Polisi na idara ya misitu, ambapo tayari mashamba yenye hekari zaidi ya sita yaliyolimwa bangi yameteketezwa.
Kingalame amesema, hayupo tayari kuona baadhi ya watu wakifanya biashara ya kulima bangi Wilayani humo na kuwataka wenye tabia hiyo kuacha mara moja.
“Wanaofanya biashara ya kulima bhangi watafute pakwenda mimi kama mkuu wa wilaya sipo tayari kuona jamii ya Nyang’hwale wanakuwa kwenye hali hatarishi kwa sababu ya mihadarati nawasihi sana tufanye kazi za maendeleo,“ amesema Kingalame.
Naye, Afisa misitu wa Wilaya hiyo, Asafu Manya amesema taarifa za uwepo wa mashamba katikati ya msitu huo zimetolewa na wasamaria wema na kuitaka jamii kuacha kuingia maeneo ya misitu na kufanya uharibifu wa mazingira kwakuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Nae hakimu wa mahakama ya wilaya ya Nyang’hwale, Daniel Nyange aliwataka wananchi kuachana na kilimo cha bangi na badala yake wajikite kwenye shughuli nyingine za kuwapatia kipato ikiwemo uchimbaji wa madini, kilimo cha mpunga na biashara.