Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili wakidaiwa kujaribu, kukata baadhi ya vyuma vya ngazi ya nguzo kwenye daraja la Tanzanite lililopo maeneo ya Salender.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4, 2022 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi, walikamatwa Aprili 02, 2022  saa  10 alfajiri wakiwa wanajaribu kufungua vyuma  vilivyopo kwenye nguzo  inayojulikana kama  P9 ambayo ipo  kwenye  daraja hilo.

Aidha watuhumiwa hao wanahojiwa kwa kina na watafikishwa kwenye vyombo vya kisheria kwa hatua zaidi pale uchunguzi utakapokamilika.

“Watuhumiwa hao   pia  wanahojiwa kwa kina ili kubaini malengo yao chini ya daraja hilo, yalikuwa ni nini na kuona kama wana uhusiano na wale waliokuwa wanajaibu kuiharibu baadhi ya miundombinu ya nguzo,” Amesema Muliro.

Hata hivyo Jeshi la Polisi linatoa onyo kali na halitamvumilia mtu au kikundi chochote kinachojihusisha kwa namna yoyote ile kujaribu kuharibu miundombinu ambayo imejengwa kwa manufaa ya umma.

Profesa Mkenda Mwalimu alikuwa mtu wa usawa
Dkt.Biteko:Madini yaongeze amani ukanda wa Maziwa Makuu