Kulingana na mtandao wa soka nchini Ghana unaofahamika kwa jina la Football Ghana, taarifa zimeeleza kuwa klabu ya Young Africans imejitosa kumuwania mshambuliaji wa Asante Kotoko Yacouba Sogne ambaye amemaliza mkataba wa kuitumikia klabu hiyo.

Awali Sogne alikuwa akitajwa kuwa mbioni kujiunga na klabu ya Medeama ya huko huko Ghana hata hivyo dili la uhamisho wake lilisitishwa baada ya Medeama kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa.

Kwa hapa Tanzania, Simba wanadaiwa kuwa klabu ya kwanza kuwasilisha ofa kumtaka mchezaji huyo lakini Young Africans wamejitosa wakiwa na ofa nono zaidi.

Kulingana na mtandao huo, ofa ya mabingwa wa soka Tanzania bara Simba SC ni dola za kimarekani 80,000 huku Young Africans wakipanda juu kwa dau la dola za kimarekani 100,000.

Aidha kuna taarifa kuwa nyota huyo pia anawaniwa na klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Katika jitihada za kuboresha kikosi chao, Young Africans wameweka mkazo katika kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, ambapo nyota kadhaa wamekuwa wakihusishwa na mabingwa hao wa kihistoria.

Washambuliaji wengine wa kigeni wanaohusishwa na Young Africans ni Heritier Makambo (Horoya AC) na Michael Sarpong (huru) baada ya kufukuzwa na uongozi wa Ryon Sports ya Rwanda.

Yikpe aomba nafasi nyingine Young Africans
Niyonzima ahamia ufukweni