Mshambuliaji wa klabu ya Young Africans Yikpe Gislain, amesema anahitaji kupewa nafasi ya mwisho katika kikosi hicho ili awaoneshe kazi, mashabiki na wanachama.

Yikpe alisajiliwa na Young Africans wakati wa dirisha dogo la usajili mwishoni mwa mwaka jana, akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Kenya Gor Mahia.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo hajaonesha kiwango kizuri cha kuwafurahisha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kongwe yenye maskani yake makuu jijini Dar es salaam, katika michezo aliyocheza ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Na mpaka sasa ameshafunga bao moja.

Mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast amesema bado ana malengo ya kuendelea kuitumikia Young Africans, na kuwa sehemu ya wachezjai watakaoipa mafanikio klabu hiyo.

Amesema anataka akiondoka katika klabu hiyo akiwa ameacha historia, hivyo akipewa nafasi ya kuaminiwa na viongozi/mashabiki ataonesha maajabu ndani ya kikosi hicho.

“Japo nimepata nafasi mara kadhaa za kuingia uwanjani, lakini sijafanya kile Yanga wanataka, imani yangu msimu ujao nitafanye makubwa zaidi,” alisema Yikpe.

Hata hivyo nyota huyo ametoa sababu ya kuonekana akicheza chini ya kiwango kwa kusema alikaa miezi sita bila kucheza soka, hivyo anaamini hali hiyo imekua kichocheo cha kuonekana hana msaada ndani ya kikosi cha Young Africans.

Amesema kocha wa timu hiyo, Luc Eymael, kabla ya ligi kusimama alikuwa anampa mazoezi makali ambayo yamefanya kiwango chake kubadilika, na sasa anaendelea kufanya mazoezi binafsi katika kipindi hiki ambacho bado Serikali inapambana na vita ya maambukizi ya virusi vya Corona.

“Kwa sasa niko fiti, ligi ikirudi na nikipewa nafasi lazima nifanye maajabu,” alisema Yikpe.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, anaendelea kufanya mazoezi ya Gym na kukimbia ufukweni asubuhi na jioni kwa lengo la kujiweka fiti.

Kagera apeleka balaa nyumbani kwa Popat
Yacouba Sogne awekwa njia panda