YANGA kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk. Jonas Tiboroha, imesema wapo tayari kumwachia kocha msaidizi wao, Charles Boniface Mkwasa, kukitumikia kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, ikilitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufuata utaratibu.
TFF wapo katika mpango wa kumpa Mkwasa mkataba wa kudumu baada ya kuridhishwa na maendeleo ya Stars tangu kuondoka kwa Mholanzi, Mart Nooij, japo hajashinda mechi hata moja kati ya tatu walizocheza.
“Tupo tayari kumwachia, TFF wafuate utaratibu wa kuvunja mkataba, ana mkataba na sisi wa miaka miwili ambao ameutumikia kwa miezi minane tu,” alisema Tiboroha.
TFF chini ya Rais Jamal Malinzi, walimteua Mkwasa kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu wa Stars kwa muda wa miezi mitatu, muda ambao unaelekea kufikia ukingoni.
Mkwasa alijikuta akizidi kujiongezea sifa baada ya wapenzi wa soka nchini kuishuhudia Stars ikicheza soka la hali ya juu dhidi ya Nigeria juzi na kutoka nayo suluhu.
Mchezo huo ulikuwa ni wa kuwania kufuzu fainali za Afrika (Afcon 2017) zitakazofanyika nchini Gabon.
Chanzo:Bingwa.

Kubenea: Dk Slaa Anajua Hoja Ya Richmond Na Lowassa Haipo, Kuna Ripoti Mbili Tofauti
Andrea Bertolacci Aondolewa Kambini