Kupitia uratibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, mwaka 2023 itajielekeza kwenye kuimarisha na kuunganisha mifumo kuanzia ngazi ya Msingi hadi Taifa, ili kuongeza nguvu ya mapambano ya kudhibiti na kutokomeza ukatili wa kijinsia na watoto.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Doroth Gwajima wakati akifungua kongamano la wanawake na uongozi lililojadili ushiriki wa wanawake katika uongozi, ili kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Doroth Gwajima akiangalia picha ya Dkt. Helen Kijo Bisimba.

Amesema, ipo haja ya kuzijengea uwezo endelevu Kamati za ulinzi wa wanawake na Watoto zilizopo, ili zifanye kazi na wadau wa jamii huku akibainisha kuwa tayari Kamati za ulinzi wa wanawake na Watoto 18,186 kati ya 20,750 zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, Kata na Kijiji kwa mwaka 2021/22.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Wadau inatambua umuhimu wa kuwa na wanawake viongozi mahiri na kuwekeza rasilimali katika usawa wa kijinsia kama chachu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Baadhi ya washiriki wakiwa katika kongamano la wanawake na uongozi lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Awali, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema kuwekeza rasilimali katika usawa wa kijinsia ni kuhakikisha kuanzia sera, mipango na bajeti zinakuwa katika mlengo wa kijinsia ambapo itachangia makundi yote kunufaika katika jamii bila kuachwa mtu nyuma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi TGNP, Gemma Akilimali aliongeza kuwa mabadiliko ya tabia nchi pia yamechangia vitendo vya ukatili wa kijinsia, hasa katika upungufu wa nishati na maji hivyo wanawake na watoto wanaathirika kwa utafutaji wa rasilimali hizo.

Biden na Macron waapa kuiwajibisha Urusi
Wataka Rais ajiuzulu au wamtoe ofisini kwa lazima