Kampuni ya Bharti Airtel, ambayo ni mmiliki wa Airtel Tanzania wamejibu ripoti iliyotolewa na Kamati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango na kueleza uhalali wa umiliki wa kampuni hiyo.

Bharti imeeleza kuwa ilifuata taratibu na sheria zote za kununua hisa na hatimaye kumiliki Airtel Tanzania, na kwamba waliishirikisha Serikali na kupata baraka katika hatua zote.

“Miamala ilifanyika kwa uwazi chini ya usimamizi wa Bodi ya Wanahisa (MSI), wawakilishi wa Benki ya Dunia, Serikali ya Uingereza, Marekani, Uholanzi na Ujerumani. Makundi hayo yalishirikishwa ili kuhakikisha kuna maadili na misingi ya utawala bora kwenye kampuni,” imeeleza taarifa hiyo.

Katika umiliki wa kampuni hiyo, Serikali sasa inamiliki asilimia 40 kupitia kampuni ya simu ya TTCL dhidi ya asilimia 60 za Bharti.

Kampuni hiyo imeonesha miamala mingi iliyofanywa mwaka 2001 katika mchakato wa kutafuta mwekezaji kupitia TTCL kwa ajili ya simu za mkononi hadi uuzwaji wa Zain kwenda Airtel.

Aidha, Katika taarifa yake baada ya kufanya uchunguzi, Dkt. Mpango alisema kuwa kilichobainika ni ‘mambo ya hovyo’ na kwamba taifa liliingizwa mkenge kwa maslahi ya watu binafsi.

“Tuliyoyaona ni mambo machafu sana, ni mambo ya hovyo kabisa. Nchi yetu kwa ufupi iliingizwa mkenge, fedha nyingi zilipotea” alisema Dkt. Mpango.

Aliongeza kuwa Serikali imeamua kufanya mazungumzo na Kampuni ya Airtel ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata haki yao.

Amchoma visu mpenzi wake akidai ‘Mungu’ amemtuma
Hongera Navykenzo kwa ka-baby