Unapokuwa kwenye tatizo la pamoja kama jahazi likielekea kuzama utasikia, “kila mtu amuombe Mungu wake”. Unaweza kujiuliza wapo wangapi, kwani tunajua ni mmoja tu. Lakini mkasa huu unaweza kukupa jibu la tangazo hilo.

Mwanaume mmoja wa Michigan ameripotiwa kumchoma visu mama wa mtoto wake wa miaka 13 akidai kuwa Mungu ndiye aliyemuagiza kufanya hivyo!

Kwa mujibu wa New York Daily News na gazeti la Battle Creek Enquirer la Michigan, vyombo vya usalama vimeeleza kuwa mwanaume huyo alitekeleza tukio hilo mbele ya mwanaye. Mtoto alipojaribu kumzuia asiendelee kumshambulia mama yake alimwambia amuache kwani ni ‘Mungu’ ndiye aliyemtuma kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa Sajenti, Todd Elliott ambaye ni kiongozi wa Idara ya Upelelezi ya eneo la Battle Creek, mshambuliaji alivamia usiku wakati mwanamke huyo alikuwa ndani amelala na watoto wake watatu, mmoja akiwa mtoto wa mwanaume huyo.

Taarifa ya polisi imeeleza kuwa alikuwa amebeba kisu chenye urefu wa futi tatu.

Mtuhumiwa alikimbia muda mfupi baada ya kutekeleza tukio hilo, lakini mtoto alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na kumtambua kisha wakamkamata siku iliyofuata.

Polisi wameeleza kuwa walikuta damu nyingi kwenye nyumba lilikofanyika tukio hilo pamoja na kisu kilichohusika. Pia, walikuta nguo za mtuhumiwa zikiwa na damu.

Mwanamke aliyeshambuliwa ameripotiwa kuwa katika hali ya mahututi akifanyiwa upasuaji kujaribu kuokoa maisha yake.

Bila shaka mungu anayemsema mtuhumiwa hapa sio Mungu wetu tunayemuamini na kumuabudu.

Video: Watanzania waombwa kuendelea kumchangia matibabu mtoto aliyefanyiwa operesheni 10 bila nafuu
Airtel wajibu ripoti ya Dkt. Mpango, wang’ang’ania uhalali