Andy Murray amefanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Wimbledon, inayoendelea jijini London nchini England baada ya kusmhinda mpinzani wake kutoka nchini Australia Nick Kyrgios.

Murray alimshinda Nick Kyrgios anaeshika namba 15 kwa ubora duniani upande wa wanaume, kwa seti tatu kwa sifuri ambazo ni 7-5 6-1 na 6-4.

Hata hivyo Kyrgios mwenye umri wa miaka 21, hakukubali kushindwa kirahisi kutokana na umahiri mkubwa aliouonyesha wa kupambana kwa ukakamavu, hali ambayo ilimfanya Murray kutumia mbinu za ziada.

Kwa ushindi huo, Murray anaeshika namba mbili kwa ubora duniani upande wa wanaume atapambana na mshiriki kutoka nchini Ufaransa Jo-Wilfried Tsonga siku ya jumatano.

Tsonga alitinga hatua ya robo fainali kwa kumshinda mfaransa mwenzake Richard Gasquet ambaye hata hivyo alishindwa kumaliza mchezo kutokana na maumivu ya mgongo yaliyokua yakimsumbua.

Kabla ya kufanya maamuzi ya kuachana na mchezo huo, Gasquet alikua nyuma kwa seti moja ambayo ni 4-2.

Michezo mingine ya hatua ya mzunguuko wa wanne kwa wanaume ilishuhudia;

Roger Federer [3] akimshinda Steve Johnson, seti tatu kwa sifuri ambazo ni 6–2, 6–3, 7–5.

Marin Čilić [9] akimshinda Kei Nishikori [5] baada ya kujioondoa mchezoni kutokana na majeraha, lakini alikua nyuma kwa seti mbili kwa sifuri ambazo ni 6–1 na 5–1.

Milos Raonic [6] akimshinda David Goffin [11], kwa seti tatu kwa mbili ambazo ni 4–6, 3–6, 6–4, 6–4 na 6–4.

Jiří Veselý  alionekana kuwa karibu kumshinda Tomáš Berdych [10], kwa kuongoza seti tatu moja 6–4, 3–6, 6–7 na 7–6 lakini baadae mchezo uliahirishwa na utamaliziwa hii leo.

Michezo mingine ya robo fainali kwa wanaume itakua kati ya;

Sam Querrey (28) kutoka nchini Marekani atapambana na Milos Raonic (6) wa Canada

Roger Federer  (3) kutoka nchini Uswiz atapambana na Marin Čilić     (9) wa Croatia

Mshindi kati ya Jiří Veselý  Vs Tomáš Berdych wote kutoka Jamuhuri ya Czech  atapambana na    Lucas Pouille (32) Wa Ufaransa

Jo-Wilfried Tsonga (12) kutoka nchini Ufaransa atapambana na Andy Murray (2) kutoka Scotland

Muhimu: kwenye mabano ni nafasi ya ubora kwa mchezaji kwa mujibu wa viwango vya dunia.

Video Mpya: Harmonize - Matatizo
Video: Mtazame mchezaji Musa Saidi wa Tanzania akipasha huko Ufaransa, COPA Camp ya 2016