Kikosi cha Azam FC huenda kikamalizia Maandalizi yake mjini Cairo, kufuatia Benchi la Ufundi la timu hiyo, kuhitaji mchezo wa Kirafiki dhidi ya Timu za Daraja la juu nchini Misri.

Juzi Jumatano (Agosti 03), Azam FC ilicheza mchezo wa pili wa Kirafiki dhidi ya Grand SC uliomalizika kwa Wakali hao wa Chamazi kuibuka na ushindi wa 1-0, huku wakipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Wadi Degla kwa kufungwa 0-1.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa klabu hiyo Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’ amesema Benchi la Ufundi limepanga kuwa na mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya klabu inayoshiriki Daraja la juu nchini humo, baada ya kucheza na klabu za madaraja ya chini kwenye michezo miwili ya awali.

Amesema Kocha Mkuu Abdihamid Moallin amesisitiza kupata timu yenye kiwango cha juu zaidi ili kuipima timu yake kabla ya kurejea Dar es salaam, tayari kwa Msimu Mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Wiki ya Kwanza Kocha alikua na jukumu la kutengeneza eneo la nyuma, Wiki ya Pili Kocha alikua na kazi ya kuijenga nafasi ya kiungo ili kupeleka nguvu katika eneo la Ushambuliaji, na ndio maana katika mchezo wetu wa Pili hilo lilionekana kwa kiwango kikubwa.”

“Amesema kwa sasa anahitaji kucheza na timu yenye viwango vya juu zaidi, kwa maana timu tuliocheza nayo juzi inashiriki Ligi Daraja la Pili hapa Misri, kwa hiyo amehitaji mchezo huo, ambao anaamini utakua ni kipimo kizuri kwa kikosi chake.”

“Kama tutafanikiwa kupata Timu ya Daraja analotaka Kocha, itatulazimu kwenda Cairo kumalizia Maandalizi yetu ya kujiandaa na Msimu mpya, ambapo huko ndipo kuna timu nyingi zenye sifa ambazo Kocha Miallin anazitaka.” amesema Zakazakazi.

Awali Azam FC ilitamani kucheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya Simba SC iliyokua imeweka Kambi mjini Ismailia-Misri, lakini mpango huo ulishindikana kutokana ratiba za timu hizo kukinzana.

Tayari Simba SC imesharejea jijini Dar es salaam, kumalizia sehemu ya Maandalizi ya Msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Edo Kumwembe: Young Africans inanipa homa
Mosimane aukubali MZIKI wa Young Afrians