Uongozi wa Azam FC umefunguka sakata la Kocha Kally Ongala kushindwa kupewa Tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi Novemba, kwa mujibu wa Takwimu ambazo zinaonesha kumbeba, tofauti na Kocha wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda.

Bodi ya Ligi Kuu ‘TPLB’ usiku wa kuamkia jana Alhamis (Desemba 08) ilimtangaza Kocha Juma Mgunda Kuwa Kocha Bora wa Mwezi, sambamba na Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Mayele aliyetajwa kama Mchezaji Bora.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdul-Karim Amin ‘Popat’ amesema wanaheshimu maamuzi yaliyotangazwa na ‘TPLB’ na hawana budi kumpongeza Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Mgunda kwa tuzo aliyoipata kutokana na kukuongoza vizuri kikosi chake kwa mwezi Novemba.

“Hatuna lolote la kulalamika, ninachukua nafasi hii kumpongeza Kocha Mgunda kwa kupewa tuzo hiyo, lakini wanaojua zaidi ni watu ambao wako kwenye hiyo kamati ambao wanachagua Kocha Bora wa mwezi, wao ndio wanajua sahihi kuliko sisi.”

“Ninachojua sisi timu yetu inapata matokeo, tumeshinda michezo minane mfululizo na tuko vizuri, tunaendelea kufanya vizuri na Mwenyezi Mungu atujaalie hivyo tuendelee mpaka mwisho wa msimu.” amesema Popat

Hata hivyo Bodi ya Ligi ‘TPBL’ imetoa sababu za kutangazwa kwa Kocha Juma Mgunda kuwa mshindi wa Tuzo ya mwezi Novemba baada ya kutoonekana kwa jina la Kocha wa Azam FC, Kally Ongala licha ya kuwa na rekodi nzuri ndani ya kikosi hicho.

Afisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda amesema sababu ya kocha wa Azam kutohusishwa kwenye tuzo hizo ni kwasababu timu hiyo ilikuwa haina kocha mkuu na kocha aliyekuwepo hana vigezo.

“Taarifa ya Azam kutohushwa kwenye tuzo za mwezi ni kwasababu timu hiyo ilikuwa haina kocha mkuu na kocha aliyekuwepo hana vigezo vya kuwa kocha mkuu wala kocha msaidizi na hatujakosea kwenye kufanya maamuzi katika hilo,” amesema Boimanda.

Ongala alikabidhiwa mikoba ya kukinoa kikosi hicho mwezi Oktoba baada ya kumtimua Dennis Lavagne na kukiongoza katika mechi nane za ligi bila kupoteza.

Azam FC chini ya Ongala imepata ushindi dhid ya Simba, Ihefu, Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting, Namungo, Coastal Union na Polisi Tanzania.

Rasmi Honour Janza aitema Namungo FC
Wadau wa Habari wataka ushirikishwaji utungaji wa Sheria