Mtangazaji mahiri wa vipindi vya burudani nchini Hamis Mandi maarufu B Dozen ameweka wazi mtazamo wake juu ya anachokiona kama chanzo cha kusuasua kwa tasnia ya muziki wa bongo fleva ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika yanayoendelea kuandika historia za kipekee kila kukicha.

Dozen amewaondoa shaka wadau wa muziki wanaohisi kuwa kwa sasa ni ngumu muziki wa Tanzania kuingia kwenye ushindani na kujipenyeza kwenye soko kubwa zaidi kwa kubainisha njia inayopaswa kufuatwa na wasanii wote nchini ili kufikia mafanikio makubwa kwenye tasnia hiyo.

“Muziki wetu unaweza kurudi kwenye nafasi ya ushindani, ila tu ni kama tutaamua kuwa kitu kimoja, niache kuona kwamba wewe ni bora kuliko mimi, tukishakuwa kitu kimoja tutaweza kuendelea mbali zaidi, na hivyo ndivyo walivyofanya wasanii wa Nigeria na South Afrika” Alisema Dozen

Kufuatia kauli hiyo ya awali Dozen ameenda mbali na kufafanua chati ya muziki wa afrika inavyokwenda inabadilika huku akigusia namna baadhi ya mataifa hasa Nigeria na Afrika kusini walivyoweza kuhakikisha  wanajiweka katika sehemu inayoubeba na kuupeleka mbali zaidi muziki na wasanii wao.

“Wasanii wa South Afrika walikuwa juu kabla ya muziki wa Nigeria, wa Nigeria wakaamua kuungana wakatengeneza terms zao wakawa kitu kimoja wakaendelea.

Nitaendelea kusimama pale pale bila umoja wa kila mmoja kumuunga mkono mwezake hatuwezi kufika mbali.”  aliongeza Dozen.

Hamis Mandi au B Dozen ni mmoja ya watangazaji wa muda mrefu wa Tanzania kwa vipindi vya burudani ya muziki ikijumuisha muziki wa kizazi kipya na muziki wa nchi za kigeni unaoendana na vijana.

Wizkid awapiga chini wasanii maarifu Afrima
Abby chams atumbuiza Expro2020 Dubai.