Mgogoro ulioanza kufukuta kwenye mitandao ya kijamii kati ya mmiliki wa makampuni ya Global Publishers, Erick Shigongo na meneja wa Diamond Platinumz, Babu Tale umechukua sura mpya  baada ya meneja huyo kudai ametishiwa.

Mtafaruku kati ya wawili hao ulianza baada ya Shigongo kuandika katika ukurasa wake wa Instagram ushauri wake kwa Diamond akidai kuwa kitendo cha kujikita katika matamasha ya kimataifa na kuyaweka kando ya ndani huku akitaka kulipwa zaidi ya shilingi milioni 100 pia ndani ya nchi kutamgharimu hususan kupoteza mashabiki wa ndani siku za usoni.

Akifunguka jana kupitia ‘Shilawadu’ ya Clouds TV, Babu Tale ambaye alimtaja Shigongo kuwa ni mtani wake kikabila, alimlalamikia kwa kudai kuwa alimpigia simu na kumweleza maneno ambayo aliyatafsiri kama vitisho.

Alidai kuwa baada ya kumpigia simu na mwandishi huyo nguli wa vitabu vya uhamasishaji wa kiuchumi na masimulizi alimuuliza ‘kama anataka vita’ kati yao baada ya maelezo.

“Nikipata matatizo leo,  ina maana aliyeniambia ‘ninataka vita’ ina maana amenisababishia matatizo. Lakini sitaishia hapa nitafuata vyombo vya sheria ili vinilinde,” alisema Babu Tale.

Meneja huyo wa WCB alionesha kushangazwa na kitendo cha Shigongo kumshauri Diamond kupitia Instagram, akidai kuwa kama angekuwa na nia njema kweli angemuita na kumshauri hata akiwa ofisini kwake.

Tale alienda mbali na kueleza kuwa Shigongo anampango wa kumuangusha katika biashara zake baada ya wawili hao kushindwana katika mambo yao ya kibiashara. Alimlaumu Shigongo pia kwa kuweka hadharani ujumbe aliomtumia kwenye simu.

Bado haijajulikana uhalisia wa chanzo cha mgogoro huo, lakini dalili zote zinaonesha huenda kukawa na msuguano wa kibiashara au kutoelewana katika hoja dhidi ya Diamond Platinumz ambaye ni bidhaa kubwa Afrika iliyo kwenye mikono ya Babu Tale na Salaam.

Video: Zitto, Chedema watifuana tena, Serikali yalainika hoja Katiba mpya
Lissu akabidhiwa zigo na Kaimu Jaji Mkuu