Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Bakari Nyundo Shime, amesema hatarajii kuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi katika mchezo dhidi ya vijana Shelisheli utakaopigwa kesho Jumamosi Julai 2, 2016 kwenye Uwanja wa Stade Linite mjini Victoria.

“Timu haitakuwa na mabadiliko makubwa. Almost kikosi kitakuwa ni kilekile cha Dar es Salaam kwa sababu nitampumzisha Job (Dickson Nickson) tu katika mchezo wa kesho, na nafasi yake atacheza Enrick (Vitalis Nkosi),” amesema Shime leo Julai 1, 2016 kabla ya kwenda kwenye mazoezi ya mwisho yatakayofanyika Uwanja wa Linite.

Shime maarufu kwa jina la Mchawi Mweusi, amesema anauchukulia mchezo huo kwa uzito uleule na kuongeza ana sababu za kiufundi na kimbinu kumpumzisha Job katika mchezo wa marudiano kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana, zitakazofanyika mwakani huko Madagascar.

Kwa hali halisi ilivyo timu iko vema na ikathibitishwa na Shime mwenyewe akisema: “Kikosi kiko vema kwa maana ya wachezaji wako vizuri na kambi iko vizuri kwa sababu hakuna majeruhi.” Pia Daktari wa timu hiyo, Shecky Francis Mngazija alithibitisha.

“Sioni kama kuna dalili zozote za hujuma na kimbinu tumejipanga vema. Tumefuta matokeo ya Dar na tuko huku tunataka matokeo mapya. Mbinu zangu siku zote ni ushindi wa nyumbani na ugenini,” amesisitiza.

Serengeti Boys ilitua kwenye Kisiwa cha Mahe uliko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Visiwa vya Shelisheli jana Juni 30, 2016 majira ya saa 11 jioni.

Timu hiyo iliyosafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia ilisafiri salama na wachezaji wote 20 wakiwa na viongozi wanane, walikuwa kwenye hali nzuri na kupokewa vema na wenyeji waliowaandalia usafiri kutoka uwanjani hapo hadi Victoria- Mji Mkuu wa nchi hii na kufikia Hoteli ya Berjaya Beau Vallon Resort iliko Kilometa 25 kutoka uwanja wa ndege.

Leo Julai mosi, itakuwa na mazoezi ya kipindi kimoja tu kwenye uwanja huo kuanzia saa 10.30 jioni (saa 9.30 kwa saa za Tanzania au Afrika Mashariki). Uwanja wa Stad Linite upo kilometa 10 kutoka hotelini.

Shime ana matumaini makubwa kuiondoa Shelisheli katika mbio hizo baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumapili ya Juni 26, 2016.

Na ili iweze kufuzu, Serengeti Boys inahitaji kusimama imara katika matokeo hayo ama kwa kupata sare ya aina yoyote, kushinda au ikitokea kupoteza, basi isifungwe zaidi ya mabao 2-0.

Katika mchezo wa Dar es Salaam waliozifumania nyavu walikuwa Nickson Kibabage, Ibrahim Abdallah na Ally Hussein ambaye alifunga kwa penalti na kila mmoja amepania kufunga kama kocha akiwapa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza.

Nyota waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm Kabwili na Samwel Edward Brazio wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba.

Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Yassin Muhidini Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Rashid Mohammed Chambo, Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima Makame Vitalis.

Serengeti Boys ambayo inahudumiwa na TFF kwa asilimia 100 ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mechi hizo za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Shelisheli na Afrika Kusini ambayo itapambana nayo baadaye mwezi ujao.

Katika kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.

Yamoto Band Hawakuona Umuhimu Wangu kwenye Video ya Su -Rubby
Video: Ajali mbaya iliyohusisha magari 3 Morogoro