Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, Fadhili Chamile ni mmoja kati ya watu sita wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya tuhuma za mauaji ya kinyozi aliyefahamika kwa majina ya Mwinyi Mpeku katika tukio lililotokea Manzese, Dar.

Tukio hilo limetokea Alfajiri ya mwanzoni mwa juma hili katika mitaa ya Manzese ambapo chanzo cha mauaji hayo yanatajwa kuwa marehemu kupigiwa kelele za mwizi, hali iliyosababisha kupokea kipigo kizito kilichosababisha mauti yake.

Taarifa za uhakika kutoka kwa watu wa karibu na eneo hilo ambao hawakutaka kutaja majina yao wameeleza kuwa kabla ya marehemu kukutwa na umauti usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu, alionekana akinywa kilevi katika moja ya baa ya eneo la Tip Top ambapo alipotoka hapo ndiyo alikutana na mauti hayo.

“Marehemu anaitwa Mwinyi na kilichotokea jamaa alikuwa anatoka kulewa na alikuwa na rafiki yake lakini wakati wapo njiani inasemekana akakutana na mdaiwa wake ambaye katika kudaiana yule mdaiwa ndiyo alianza kumuitia mwizi na hiyo ilikuwa ni muda wa saa 11 kwenda 12 asubuhi.”

“Sasa katika kumpiga ndiyo vijana wa bodaboda wanaopaki katika eneo lilipotokea tukio ambao wanatajwa kushiriki akiwemo huyo Chamile ingawa baadae walitokea watu wanaomjua wakamtetea na kulipombazuka alijikongoja kwake kabla ya kuzidiwa na kupelekwa Palestina na Mwanayamala alipokataliwa.”

“Akapelekwa Muhimbili na baada ya vipimo ikaonekana ubongo umechanganyika na damu na jioni ndio zikatoka taarifa za kuwa amefariki lakini kabla ya taarifa za msiba Chamile na vijana wengine wa bodaboda walikuwa tayari wameshakamatwa, marehemu alizikwa Jumanne,” amesema mtoa taarifa hizi.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, mmoja ya viongozi wa juu wa jeshi hilo ambaye jina lake hakutaka liandikwe alisema: “Ni kweli anashikiliwa, alikuwepo Kituo cha Urafiki lakini amehamishwa Kituo cha Mburahati, yupo na wenzake watatu na bado tunaendelea kuwatafuta wengine, uchunguzi tayari umeanza ndiyo maana wanashikiliwa.”

Tafsiri maboresho sheria ya madini, GGML ni mfano: Dkt. Kiruswa
Kocha US Monastir aitega Young Africans