Serikali ya Burundi imejikuta kwenye wakati mgumu mbele ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, kufuatia tuhuma za kuiondoa nchini humo timu maalum iliyotumwa, kabla ya kukamilisha kazi yake mwezi Machi mwaka huu.

Balozi wa Burundi aliyekuwa jijini Geneva, Switzerland alipata wakati mgumu wa kujieleza baada ya Kamishna Msaidizi wa Tume ya Haki za Binadamu, Kate Gilmore kueleza kuwa timu yake ilishindwa kukamilisha ripoti ya kuchunguza vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo baada ya kukataliwa kuongeza muda.

Alisema Serikali iliwazuia kuendelea na kazi hiyo, ingawa awali Serikali na Umoja wa Mataifa walikubaliana kuwa timu hiyo itafanya kazi na itapewa ushirikiano wa kutosha.

“Ni dhahiri kuwa kufuatia kutoonesha ushirikiano kwa timu yetu, tumeshindwa kuwasilisha katika baraza hili ripoti ya uchunguzi wa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi,” alisema.

Aliongeza kuwa timu ya wataalam iliyoingia nchini humo iliambiwa na Serikali kuwa ‘visa’ zao zimekwisha na kwamba hawataruhusiwa kuongeza muda hadi Aprili, tofauti na makubaliano ya awali.

Akijibu tuhuma hizo, Balozi wa Burundi alieleza kuwa anasikitishwa na maelezo yaliyotolewa kwani yanaonekana kama vile Serikali haikutoa ushirikiano kabisa, wakati kulikuwa na sintofahamu ya kilichokuwa kinafanyika.

“Burundi inasikitishwa na tuhuma hizi zisizo sawa ambazo zimeongeza chuki dhidi ya nchi yetu kwa wakati fulani,” alisema.

Alifafanua kuwa timu iliyotumwa ilibadili adidu za rejea za kazi husika, jambo ambalo liliishangaza idara ya uhamiaji ambayo ilighaili kuongeza muda wa visa za wajumbe wa timu hiyo.

Wiki iliyopita, Idara ya Uchunguzi iliyo chini ya Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa bado kuna vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi.

Muna amkana anayedaiwa kuwa mwanaye
Profesa afariki ghafla akizungumzia maisha yake kwenye TV

Comments

comments