Timu ya Coastal Union imeendelea kuziduwaza timu kubwa za Ligi Kuu nchini baada ya kuing’oa Mtibwa Sugar katika Kombe la Shirikisho baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika mchezo huo, wenyeji walilazimika kucheza pungufu kufuatia mlinzi wao, Yusuph Chuma kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kupinga maamuzi ya refa katika dakika ya 72.

Mtibwa walitumia upungufu huo wa Coastal kwa kufanya mashambulizi mfululizo lakini walinzi na viungo wa Coastal walijituma kwa juhudi zote kuzuia bao la kusawazisha.

Coastal walioanza pambano kwa kasi na kupata kona tatu ndani ya robo saa ya kwanza walijipatia bao pekee na la ushindi kupitia kwa mshambuliaji Mbwana Mshindo aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona.

Mtibwa walizinduka dakika ya 30 wakati Mohamed Ibrahim alipoipangua ngome ya Coastal na kuachia shuti kali lililopanguliwa na kipa Abubakar Abbas.

Dakika ya 85, Shiza Kichuya wa Mtibwa alishuhudia mkwaju wake wa adhabu ukipanguliwa kwa mkono mmoja na mlinda mlango Abbas na kuwa kona iliyoishia kuokolewa na walinzi wa Coastal.

Hadi dakika tisini zinamalizika, bao la Mshindo lilidumu na kuwapeleka Coastal Union katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho.

 

Habari Mpasuko: Infantino awa Rais mpya wa FIFA
Mawaziri wa Magufuli wanusurika ‘kutumbuliwa jipu’, Ikulu yanena