Klabu ya Coastal Union imekanusha taarifa za kuwa mbioni kumpa ajira Kocha Mzawa Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, baada ya kuachna na Kocha Yusuph Chipo.

Coastal Union kwa sasa ipo chini ya Kocha Joseph Lazaro anaekaimu nafasi ya Kocha Mkuu, huku Uongozi wa Klabu hiyo ukiendelea na mchakato wa kumsaka Mbadala wa Chipo.

Afisa Habari wa Klabu hiyo yenye maskani yake jijini Tanga Jonathan Tito amesema, taarifa za Coastal Union kuhusishwa na Julio ni mapema mno kuzithibitisha kwa sasa, lakini amesisitiza mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu mpya utakapokamilika utawekwa hadharani.

“Siwezi kuzungumza au kuthibitisha tetesi hiyo kwa sasa, kwa sababu bado hakuna taarifa rasmi kutoka uongozi wa juu.”

“Kwa maana hiyo nakataa hili suala la Kocha Julio kuwa Kocha Mkuu wa klabu yetu, mpaka pale taarifa rasmi itakapotoka.”

Coastal Union imekua na mwenendo mbaya katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikicheza michezo 22 hadi sasa.

Ukomo magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni 2030
Waandishi watatu wa TV wafutwa kazi kwa kulikejeli Bunge