Klabu ya Crystal Palace imekubali ada ya Pauni milioni 32 iliyoombwa na uongozi wa klabu ya Liverpool kwa ajili ya usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Christian Benteke.

Taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya Sky Sports zimeeleza kuwa, Palace wamekubali kulipa ada hiyo, baada ya ofa yao ya awali ya Pauni milioni 23 kukataliwa.

Kwa mantiki hiyo sasa Benteke anaingia katika historia ya klabu ya Crystal Palace ya kuwa mchezaji ghali ndani ya klabu hiyo ya jijini London, ambayo haikuwahi kufanya usajili wa mchezaji kwa zaidi ya pauni milion 25.

Liverpool walimsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kwa kiasi cha Pauni milioni 32.5 mwaka mmoja uliopita akitokea Aston Villa, lakini tangu alipowasili meneja Jurgen Klopp amekua na wakati mgumu wa kucheza katika kikosi cha kwanza.

Hata hivyo meneja huyo kutoka nchini Ujerumani, amekua msaada mkubwa kwa Liverpool katika biashara ya kuuzwa kwa Benteke kutokana na kupinga ofa ambazo ziliwahi kutumwa klabuni hapo.

Mpango wa usajili wa Benteke, unatarajiwa kumsaidia meneja wa Crystal Palace Alan Pardew ambaye kwa sasa anawategemea washambuliaji watatu Emmanuel Adebayor, Dwight Gayle pamoja na Marouane Chamakh.

Pia anatarajiwa kutumia kiasi cha Pauni milioni 28, alizozipata baada ya kumuuza mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Yannick Bolasie kwenye klabu ya Everton, kama sehemu ya pesa ambazo ataziwasilisha Anfield ili akamilishe mpango wa kumiliki Benteke.

Video: Kuna watu wanaona ukuu wa idara ndiyo kila kitu - Waziri Mkuu
Museveni awataka wapinzani wake kushika nyaya zenye umeme