Klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi huenda ikamsajili beki wa klabu ya Manchester United, Daley Blind baada ya kuwa kwenye wakati mgumu kukamilisha mpango wa uhamisho wa beki kutoka nchini Argentina na klabu ya Boca Juniors, Lisandro Magallan.

Meneja wa klabu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya pili msimu wa 2017/18, Erik ten amesema wanafikiria kumsajili Blind kutokana na kuufahamu vyema mfumo unaotumika klabuni hapo.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 28, alikuzwa klabuni hapo kupitia mfumo wa kuendeleza vipaji vya vijana, na anaaminiwa kama atarejea, atakuwa na uwezo mzuri wa kuisaidia timu baada ya mipango ya usajili wa beki Magallan kuwa kwenye wakati mgumu.

“Tunafanya juhudu kubwa kuhakikisha tunamrejesha Blind hapa, tunajua itakuwa kazi ya ziada kufanikisha mpango huo,” alisema Ten alipohojiwa na Sky Sports.

“Bado yupo katika taswira ya klabu hii, tangu alipoondoka tumekuwa tukiona namna alivyokua na msaada mkubwa na timu yetu. Ninaamini umefikia wakati wa kupambana ili tumrudishe,” aliongeza Ten.

Katika hatua nyingine Ten amesisitiza bado uongozi wa klabu ya Ajax haujakata tamaa katika mpango wa kumsajili beki Magallan, licha ya kupata wakati mgumu katika kipindi hiki.

Beki Magallan mwenye umri wa miaka 24 amekua na klabu ya Boca Juniors tangu mwaka 2012, na msimu uliopita alisaidia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya klabu hiyo kutetea taji la ligi.

“Hatujakata tamaa na usajili wa Magallan, tutapambana hadi tujiridhishe tumeshindwa kabisa. Lakini wakati tunafanya hivyo harakati za kumrejesha Blind nazo zitakuwa zikiendelea.”

Blind, aliihama Ajax mwaka 2014 na kujiunga na Man Utd ilipokua chini ya utawala wa meneja Louis Van Gaal, lakini tangu alipowasili Jose Mourinho amekua hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara, jambo ambalo uongozi wa klabu hiyo ya Uholanzi unaamini huenda likawawezesha kumpata na kumrejesha kwa urahisi.

Lugola: Bodaboda dawa yenu inachemka, aja na mwarobaini kupunguza ajali
Jurgen Klopp atangaza nia kwa Domagoj Vida

Comments

comments