Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Deogratius Ndejembi amekifunga Chuo cha Ualimu cha Nkuruma kilichopo Mkoka na kuagiza uongozi wa chuo hicho kurudisha fedha zote za ada walizolipa wanafunzi ili ziwasaidie kulipia vyuo vingine.
Ametoa agizo hilo wakati wa mkutano na wanafunzi pamoja na uongozi wa chuo hicho kuhusu kutafuta suluhu ya mgogoro ambao ulianza Septemba 16, mwaka huu. Chuo hicho kilidahili wanafunzi 77 kwa lengo la kufundisha kozi ya ualimu,lakini mara baada ya kuwasili chuoni hapo  waliambiwa  wanabadilishiwa masomo wasome masomo ya Maendeleo ya Jamii.Ndejembi amechukua hatua hiyo ya kukifunga chuo hicho  kutokana na wanafunzi kugoma kufanya mitihani ya chuo ya kumaliza mwaka wa masomo kwa madai chuo hakitambuliwi na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Amesema kuwa kukifungia chuo pekee haitoshi wanatakiwa kurudisha fedha zote za ada walizolipwa na wanafunzi katika mwaka huo wa masomo uliopita ili kuwasaidia kulipa vyuo vingine.

“Kuwarudishia fedha sio mwisho wa jambo hili kwa sababu mmepotezewa muda wenu na haki yenu ,mmeonewa, mmedhulumiwa kwa kusema hivyo namwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya na timu yake kuwakamata sasa hivi na wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria ili haki iweze kutendeka,” alisema Ndejembi.

Amewataja wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kuwa ni mmiliki wa chuo hicho Mathew Nkurlu, Msajili wa Chuo Yohana Michael, Mhasibu Elieth Ruben, wakufunzi Pendael Petro na Christopher Mabatian.

Ndejembi ametaja  sababu za kuagiza wakamatwe viongozi hao wa chuo ni kuwa walihusika kushiriki katika kufanya udanganyifu na kuwatapeli wanafunzi hao huku wakijua kinachoendelea.

Aidha, ameongeza kuwa serikali itawasaidia wanafunzi hao  kufanya utaratibu wa kupata vyuo vingine kwa wale wenye sifa za kujiunga na vyuo katika kozi ambayo walianza kusoma, hata hivyo amesema kama ikitokea chuo hicho kikakosa fedha za kuwarudishia wanafunzi hao, majengo yao yatatumika kama dhamana ya ada kwa vyuo ambavyo vitawapokea wanafunzi.

Video: Ahadi ya JPM kwa wananchi wa Magomeni Kota kuanza.
Mwanafunzi asimulia alivyopigwa tena baada ya kinachoonekana kwenye video ‘nilitokwa damu’