Mtangazaji na mpakuaji miziki wa kituo cha redio cha Capital FM nchini Kenya, Alex Nderi almaarufu DJ Lithium ameaga dunia.

DJ Lithium anayedaiwa kujiua kazini kwa kunywa sumu katika ofisi za kituo hicho jijini Nairobi.

Wafanyakazi wenzake wanasemekana kumkuta akiwa amepoteza fahamu dakika chache baada ya kubugia kemikali hiyo na kita msaada msaada mara moja, kumkimbiza katika Hospitali ya Nairobi.

Madaktari walimshughulikia lakini juhudi zao zikagonga mwamba baada ya kushindwa kumuamsha ikiwa dhahiri kuwa alikuwa ameondoka duniani.

Nderi anadaiwa kufuta kurasa zake zote katika mitandao ya kijamii kabla ya kujitoa uhai huku pia akiacha barua ambayo wafanyakazi wenzake wamefichua kuwa itafunguliwa na ndugu na jamaa zake.

Tukio hilo pia limethibitishwa na Kamanda wa kituo cha polisi cha Kilimani Muturi Mbogo ambaye vilevile amedokeza kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inalifuatilia suala hilo.

Mbogo amesema kuwa mwili wake umepelekwa katika chumba cha hifadhi ya maiti ya Lee ambako upasuaji utafanywa kubaini chanzo cha kifo hicho.

Kwa mujibu wa takwimu za Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya (NPS), zaidi ya watu 500 walijitoa uhai katika miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2021.

Hivi karibuni visa na matukio ya watu kujiua kwa namna tofauti vimeongezeka katika huku wito wa kuangazia afya ya akili ya wananchi wa mataifa mbalimbali ukitolewa na wataalamu wa masuala ya kisaikolojia ikithibitishwa kuwa takwimu hizo zinaongezeka pakubwa huenda kutokana na athari za janga la Korona.

Kibu Denis, Mkude kuikosa Mtibwa Sugar
BREAKING: CCM yampitisha Dkt. Tulia pekee uspika wa Bunge