Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepewa miezi mitatu kuanzia sasa kuhakikisha kuwa mkandarasi wa ujenzi wa mita za kupimia mafuta (Flow meter) anapatikana na kuanza kazi mara moja.

Agizo hilo limetolewa mapema hii leo jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Bandari ya Dar es salaam na kusisitiza kuwa mradi huo unatakiwa umalizike ndani ya mwaka mmoja.

“Hakikisheni mnaongea lugha inayofanana kati yenu na mtengenezaji ili kuepuka ucheleweshaji wa mradi huu ambao una tija kwa Taifa, pia hakikisheni mnapeleka wataalam nje ya nchi ili kuwajengea uwezo na kuongozea ujuzi na maarifa katika kusaidia kutekeleza mradi huu”, amesema Eng. Ngonyani.

Ameongeza kuwa suala la ‘Flow Meter’, ni la ushirikiano kati ya Mamlaka hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wadau wengine wa mafuta, hivyo kukamilika kwake kutasaidia na kurahisisha ukusanyaji wa mapato yatakayosaidia kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amemhakikishia Naibu Waziri Ngonyani kutatua changamoto za Mamlaka hiyo na kutekeleza agizo la ujenzi wa flow meter mara moja.

Hata hivyo,  ameongeza kuwa TPA imetoa taarifa kwa Taasisi na Idara zote za Umma ambazo zinaagiza mizigo nje ya nchi kufanya mawasiliano na Mamlaka hiyo mapema kwa mizigo ambayo ni tofauti na ile ya kawaida ili kuongeza udhibiti na usalama wa mizigo hiyo.

 

Tim Krul akaribia mlango wa kutokea St James' Park
Kushuhudia Mtanange wa Simba Vs Young Africans Shilingi 7000