Nguli wa muziki wa hip hop nchini, Fid Q anatarajia kutoa albam mbili kwa pamoja hivi karibuni, ikiwa ni sehemu ya kulipa fadhila kwa mashabiki wake ambao wamesubiri albam yake mpya kwa muda mrefu.

Ngosha ambaye wiki iliyopita aliachia ngoma mbili kwa mpigo, ‘Fresh na Ndimi Mbili’ amesema kuwa albam yake aliyoiahidi miaka kadhaa iliyopita ya ‘Kitaaolojia’ iko imekamilika na itakuwa ya kwanza kuingia sokoni.

“KitaaoloJia itakuja na ‘Kitaalegend’ ambayo itakuwa na ngoma bonus (ziada) ambazo hazikukidhi vigezo kuwepo kwenye kitaaolojia,” Fid ameiambia Clouds FM.

Katika hatua nyingine, Fid amesema kuwa anafikiria kuachia upya albam yake ya kwanza ya ‘Vina Mwanzo Kati na Mwisho’ kwa sababu watu wengi hawakuipata na amekuwa akipokea maombi ya mashabiki wengi.

“Ujue vina kati na mwisho watu wengi walikuwa hawajaishtukia ndo ile albam yenye Agosti 13,Mwanza Mwanza, kadi na Ua Rose and so on. Kwasababu ya ubovu wa soko hatukutoa kopi nyingi, lakini sasa hivi tupo kwenye ‘digital’ nitaiweka kwenye Itunes watu wengi waipate,” amesema Fid Q.

Kwa muda mrefu Ngosha alikuwa amewaweka mguu sawa mashabiki wake kuisubiri albam yake ya ‘Kitaaolojia’ ambayo inatarajiwa kuwa na nguvu kubwa.

Odinga amuweka njiapanda Kenyatta, sasa mambo yaiva
Magazeti ya Tanzania leo Agosti 19, 2017