Taasisi ya Policy Forum imefanya uchambuzi wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa ngazi ya vijiji na vitongoji ya mwaka 2019. na kuainisha makosa 13 yanayoweza kumpelekea mtu kupata adhabu katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufanyika Novemba 24.

Adhabu ambazo zimetajwa kwenye sheria hiyo endapo mtu atakutwa na hatia ni kulipa faini isiyozidi laki tatu au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja.

Kuharibu orodha ya wapigakura au nyaraka zozote zinazohusiana na uchaguzi huo ni kati ya makosa yaliyoainishwa kwenye kanuni za uchaguzi za uchaguzi wa serikali za mitaa ngazi ya vijiji na vitongoji ya mwaka 2019.

Kutoa taarifa za uongo ili kupiga kura na kujiandikisha au kupiga kura zaidi ya mara moja ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 45 cha mamlaka za Wilaya, vijiji na mamlaka za miji pamoja na kifungu cha 45 cha mamlaka za Wilaya – kitongoji.

Makosa mengine ambayo hautakiwi kuyafanya siku hiyo ni Kutishia wapiga kura au wagombea ili kuvuruga uchaguzi, kufanya kampeni siku ya uchaguzi, kuonyesha ishara au kuvaa mavazi yanayoashiria kumtambulisha mgombea au chama cha siasa katika eneo la mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura.

Kumzuia msimamizi wa uchaguzi, msimamizi wa kituo, mjumbe wa kamati ya rufaa au ofisa wa umma aliyeteuliwa kusimamia uchaguzi kutekeleza majukumu yake ni kosa kwenye kanuni ya mwaka 2019.

Kanuni hiyo inataja makosa mengine kuwa ni wasimamizi wa uchaguzi kukiuka masharti ya kiapo chao, kupatikana na karatasi za kupiga kura zaidi ya moja kwa nafasi moja inayogombewa na kuvuruga ratiba ya mikutano ya kampeni.

Ni kinyume cha kanuni hiyo kwa mtu kukutwa na na silaha kinyume na sheria kwenye eneo la uteuzi wa wagombea, mikutano ya kampeni, eneo la usikilizaji wa rufaa za wagombea, kituo cha kuandikishia wapiga kura au kituo cha kuhesabu kura na kupiga kura.

Kosa jingine ni kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla hayajatangazwa na msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa kituo.

Aidha miongoni mwa waliotoa maoni juu ya kanuni hizo ni Naibu katibu mkuu wa Chadema -Zanzibar, Salum Mwalimu ambaye ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa yapo mambo hayako sawa katika kanuni hizo jambo ambalo liliwafanya kuomba ufafanuzi wa ziada kutoka TAMISEMI ili kujua msingi wake.

Kwa upande wake Katibu wa vijana wa CCM Mkoa wa Dar es salaam, Antony Kantara amesema wananchi wengi wanazijua kanuni hizo na wamekuwa wakizitumia hata kwenye chaguzi zilizopita.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 27, 2019
LIVE: Rais Magufuli akipokea Ndege mpya Boeing 787-8 Dreamliner