Baada ya kutambulishwa kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC, Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Othos Baleke, amefunguka na kuahidi mambo makubwa.

Baleke amesajiliwa Simba SC kwa mkataba wa mkopo akitopkea Tp Mazembe ya DR Congo, ambayo mwanzoni mwa msimu huu (2022/23) ilimpeleka kwa mkopo Lebanon kuitumikia Klabu ya Nejmeh SC.

Mshambuliaji huyo amefunguka baada ya kutambulishwa jana Jumatano (Januari 18), Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kuanza kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba SC dhidi ya Mbeya City.

Baleke amesema anaifahamu vizuri Simba SC na baadhi ya wachezaji waliowakuta klabuni hapo ambao amekiri wana kiwango kizuri, huku akimini uwepo wake utaongeza kitu na kuiwezesha klabu hiyo kufika mbali katika Michuano ya Kimataifa.

“Moses Phiri mwenye mabao kumi namfahamu na wachezaji wengine kama Clatous Chama naelewa wapo kwenye viwango bora ila naamini nikiongezeka na mimi tutakuwa na uimara zaidi ya wakati huu,”

“Kabla ya kusajili niliwaambia viongozi, sitamani tena kucheza TP Mazembe, nataka kuja Simba SC ili kuonyesha makali yangu haswa kwenye eneo la kufunga ili timu iweze kufanikiwa kwenye mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa,”

“Naamini kwenye ushindani na changamoto ya kuwania nafasi ya kucheza, wachezaji wanaotumika kwenye eneo hilo la ushambuliaji kila mmoja atakaeonyesha uwezo wake mazoezini naimani Benchi la Ufundi litatoa nafasi kwa aliyefanya vizuri,”

“Ukiangalia ubora na aina ya wachezaji wa Simba SC naamini tunakwenda kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ndiyo maana nikakubali kujiunga nao.”

“Kuna kitu ninacho kwenye uwezo wangu hadi Simba SC kuvutiwa kunisajili, basi nitapambana na naamini nitaweza kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara.”

“Siwezi kueleza nitamaliza na msimu nikiwa na mabao mangapi, ila jambo kubwa nimekuja kuisaidia timu na kufanya vizuri katika kila mchezo ambao nitapata nafasi ya kucheza na hilo naamini linawezekana.”

Katika hatua nyingine, Baleke amesema alipata nafasi ya kuangalia baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, na anazifahamu timu mbalimbali, kama Young Africans na Azam FC na aina ya wachezaji waliyokuwa nao.

“Namuomba Mungu anitangulie kwenye changamoto hii mpya, kwani malengo yangu ni kuja kufanya vizuri na kuipa mafanikio timu pamoja na furaha kwa mashabiki wake, nimewaona Azam FC na Young Africans nawafahamu wote,” amesema Baleke aliyewahi kuifunga Simba SC kwenye mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki, Uwanja wa Benjamin Mkapa akiwa na TP Mazembe.

Wachezaji wengine waliosajiliwa SC wakati wa DIrisha Dogo ni Saido Ntibazonkiza (Burundi), Ismail Sawadogo (Burkina Faso) na Mohamed Mussa (Zanzibar).

Mkakati kupunguza vifo vya uzazi mama na mtoto waandaliwa
PAC yawatimua kikaoni wafanyakazi wa Wizara